Mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani waanza Davos

(CRI Online) Januari 17, 2023

Mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) umefunguliwa Jumatatu huko Davos, Uswisi, ukilenga kushughulikia tofauti na migawanyiko katika kukabiliana na misukosuko mbalimbali.

Kabla ya mkutano huo kuanza, mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wa WEF Klaus Schwab alisema nguvu za kisiasa, kiuchumi, na kijamii zinasababisha kuongezeka kwa migawanyiko katika ngazi ya kimataifa na kitaifa. Schwab alisisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta za kibiashara. "Wakati huo huo ni lazima kutambua kwamba maendeleo ya kiuchumi yanahitaji kuimarishwa ili kuwa thabiti zaidi, endelevu zaidi na hakuna anayepaswa kuachwa nyuma."

Chini ya kauli mbiu ya "Ushirikiano katika Dunia Inayogawanyika," mkutano huo wa kila mwaka utaangazia suluhu na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kukabiliana na changamoto kubwa zaidi duniani. Viongozi mbalimbali duniani watajadili masuala ikiwa ni pamoja na nishati, tabianchi, mazingira ya asili, uchumi, teknolojia, jamii, afya, na ushirikiano wa siasa za kijiografia.

Habari nyingine zinasema, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amefuta ziara yake ya kuhudhuria mkutano huo huko Davos ili kushughulikia msukosuko wa nishati nchini humo. Afrika Kusini imekuwa ikishuhudia umeme kukatika, na wakati mwingine kwa saa zaidi ya sita kwa siku.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha