Soko la usafiri nchini China kurejea kwa nguvu wakati wa likizo ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 18, 2023

Msichana mdogo akimpa babu yake salamu ya kugongeana viganja vya mikono alipokuja kumpokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kunming Changshui huko Kunming, Mkoa wa Yunnan Kusini-Magharibi mwa China, Januari 15, 2023. (Xinhua/Jiang Wenyao)

SHANGHAI - China itashuhudia likizo ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China yenye idadi kubwa ya wasafiri ambayo haijashuhudiwa katika kipindi cha miaka mitatu, huku shughuli za utalii wa ndani zikiongezeka na shughuli za utalii wa kwenda nje ya nchi zikifufuka, takwimu kutoka kwenye majukwaa ya mtandaoni zinaonyesha.

Huku watu wakirejea nyumbani kwa kujumuika pamoja na familia, usafiri wa kati ya mikoa unaongezeka wakati wa likizo ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China. Watu wengi pia wamepanga kufanya safari za masafa marefu, ambazo zimekuwa rahisi zaidi baada ya China kupunguza kwa kiasi kikubwa hatua za kukabiliana na UVIKO-19.

Takwimu kutoka Jukwaa la Trip.com zinaonyesha kuwa oda za usafiri wa masafa marefu wakati wa likizo ya sikukuu hiyo zimechangia asilimia 70 ya oda zote za usafiri wa sikukuu za kampuni hiyo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 kuliko mwaka jana.

Usafiri wa masafa mafupi, unaopendelewa zaidi wakati wa janga hili, unaendelea kukaribishwa na watalii wakati wa likizo hii. Watu wakirudi katika maskani yao wanapenda zaidi kufanya usafiri wa masafa mafupi kwenye maeneo yenye mandhari nzuri karibu na miji midogo.

Vile vile, usafiri wa kwenda nje ya China unapokea uangalizi unaoongezeka kwenye mifumo mbalimbali ya usafiri, kwa kuwa mwitikio wa China ulioboreshwa wa UVIKO-19 umeondoa vizuizi kwa usafiri wa nje ya nchi na kukuza mawasiliano kati ya watu kwenye maeneo ya mipakani.

Takwimu kutoka kwenye Jukwaa la Trip.com zinaonyesha kuwa mahitaji ya tiketi za ndege kwenda Macao wakati wa likizo yaliongezeka kwa asilimia 97 kuliko zile za likizo iliyopita, na mahitaji ya hoteli yaliongezeka kwa asilimia 57. Idadi ya oda za tiketi za ndege kutoka China Bara hadi Hong Kong nayo imeongezeka kwa zaidi ya mara 31 kuliko mwaka jana.

Wakati watu wengi zaidi wanakadiriwa kusafiri nje ya nchi baadaye mwaka huu, waendeshaji wa sekta ya usafiri na taasisi za uwekezaji zitaongeza imani katika kufufuka kwa sekta hiyo, amesema Dai Bin, Mkuu wa Taasisi ya Utalii ya China.    

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha