Wanaanga wa China watuma salamu za Mwaka Mpya wa Jadi wa China wakiwa kwenye kituo cha anga ya juu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 22, 2023

Picha iliyopigwa kwenye video ikionesha wanaanga wa Chombo cha Anga ya Juu cha Shenzhou-15, Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu wakituma salamu za Mwaka Mpya wa Jadi wa China kutoka Kituo cha Anga ya Juu cha China, Tiangong kwa njia ya video iliyotolewa na Idara ya Anga ya Juu ya China (CMSA) usiku wa kuamkia mwaka mpya.

BEIJING - Wanaanga wa China wa Chombo cha Anga ya Juu cha Shenzhou-15 Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu wametuma salamu zao za Mwaka Mpya wa Jadi wa China kutoka kwenye kituo cha anga ya juu cha China cha Tiangong katika video iliyotolewa na Idara ya Anga ya Juu ya China (CMSA) Siku ya Mkesha wa Mwaka Mpya wa jadi.

Wanaanga hao watatu, wakiwa wamevalia suti za kuruka za rangi ya samawati na rangi nyekundu iliyokolea, kila mmoja alishika karatasi yenye neno au maneno ya kutakia heri na Baraka Andiko la neno moja la Kichina "fu", likimaanisha bahati nzuri, na maandiko manne ya Kichina yanasema: kutoa salamu za heri na baraka kutoka kituo hicho cha Tiangong.

"Kuvaa nguo mpya, kula dumplings na kutakiana heria na baraka – mila na desturi na mazingira ya sherehe ni sawa hapa," amesema Zhang.

Wanaanga hao wametumia mapambo mekundu na mafundo ya Kichina kwa kupamba kituo hicho cha anga ya juu kinachozunguka, karibu kwenye umbali wa kilomita 400 juu ya Dunia.

"Ninaamini kwamba, kwa sasa, watu wengi wako zamu kwenye nafasi zao za kazi kama sisi, ambayo pia ni aina ya furaha," amesema Deng, na kuongeza kuwa ndoto na juhudi za kila mtu zinaweza kuunganishwa na kuwa nguvu kubwa ya kuhimiza msukumo wa maendeleo ya kisasa ya nchi.

Fei, ambaye ni kamanda wa misheni hiyo, ameitakia nchi na watu wake amani na ustawi.

Katika video nyingine iliyotolewa pia na CMSA Jumamosi, wanaanga hao walionyesha picha 40 zilizochorwa na watoto katika "maonyesho ya uchoraji wa anga ya juu" kama zawadi ya Mwaka Mpya kwa watu wote wa China.

Picha hizo zilirushwa pamoja na wanaanga katika siku ya kurushwa kwa Chombo cha Shenzhou-15 Novemba 29 mwaka jana, zinaonyesha hisia na matarajio ya watoto juu ya maendeleo ya haraka ya China, mila na desturi za kitamaduni na utafiti wa kishujaa kwenye anga ya juu.

Jukumu la Shenzhou-15 linakamilisha hatua ya mwisho ya ujenzi wa kituo cha anga ya juu na kuanza hatua ya kwanza ya utumiaji na maendeleo yake. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha