

Lugha Nyingine
Treni ya mizigo ya kwenda na kurudi kati ya China-Laos-Thailand yazinduliwa kutoka Yunnan, China
Picha hii iliyopigwa Tarehe 24 Novemba 2022 ikionyesha treni ya mizigo ikiingia kwenye Handaki la Reli ya Urafiki wa China-Laos inayounganisha Mji wa Mohan, Mkoa wa Yunnan, Kusini-Magharibi mwa wa China na Boten, Kaskazini mwa Laos. (Xinhua/Hu Chao)
KUNMING - Treni ya mizigo inayobeba makontena 19 yenye mfumo wa jokofu yakiwa yamepakia takriban tani 280 za mboga mboga iliondoka Kunming, Mji Mkuu wa Mkoa wa Yunnan, Kusini Magharibi mwa China, Jumanne.
Hii ni treni ya kwanza ya mizigo ya kwenda na kurudi kati ya China-Laos-Thailand. Treni hiyo ilitarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok katika muda wa ndani ya saa 55.
Itasimama kwanza kwenye Stesheni ya Reli ya Vientiane Kusini mwa Laos ili kupakia bidhaa nyingine, na kisha kuelekea Bangkok kupitia reli ya Thai, ambayo inasaidia kufupisha muda wa kusafiri kwa takriban siku moja ikilinganishwa na njia ya awali, huku pia ikipunguza gharama ya usafiri kwa zaidi ya asilimia 20, limesema Shirika la Reli la China, Tawi la Kunming. Njia ya awali ya reli ilikuwa mchanganyiko wa reli na barabara kuu.
Wakati treni hiyo itakaporudi, itabeba matunda ya msimu kama vile longan ya Thai na durian.
Kwa sasa, usafirishaji wa mizigo wa kuvuka mpaka kupitia Reli ya China-Laos unahusisha nchi za Laos, Thailand, Myanmar na nchi nyingine kwenye Ukanda Mmoja, Njia Moja. Aina mbalimbali za bidhaa zinazosafirishwa zimeongezeka kutoka aina zaidi ya 10 tu wakati reli hiyo ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza hadi aina zaidi ya 1,200 hivi sasa. Jumla ya kiasi cha mizigo kwenye njia hii sasa kinazidi tani milioni 2.5.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma