Ofisa wa afya wa Ghana apongeza Timu ya Madaktari wa China kwa kulinda afya na maisha ya watu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 17, 2023

ACCRA - Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Asilia na Tiba Mbadala wa Wizara ya Afya ya Ghana, Anastasia Michaelina Alhamisi amesifu Timu ya 11 ya Madaktari wa China nchini Ghana ambayo inakaribia kumaliza muda wa kazi yake mwezi Machi kwa juhudi zao za kulinda afya na maisha ya watu wa Ghana.

Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano yaliyofanyika mjini Accra, Ghana, Michaelina amesema kuwa madaktari hao wa China wamejitahidi kuokoa maisha ya watu na kutoa ujuzi unaohitajika kwa madaktari wenzao wa Ghana.

"Timu hii ina madaktari wa daraja la juu kutoka Mkoa wa Guangdong wa China, na utaalamu wao na akili vimechangia sana kazi ya idara za afya za Ghana, na wamefanya kazi nzuri," amesema.

Mkurugenzi huyo pia amesema timu hiyo imefanikiwa kuanzisha huduma ya upasuaji wa laparoscopic katika Hospitali ya LEKMA ilipo timu hiyo, ambayo imesaidia wagonjwa wengi kupona kwa kasi.

“Timu hiyo pia imeanzisha upasuaji wa bure kwa Waghana maskini wanaougua ugonjwa wa mtoto wa jicho chini ya mradi wa hisani, ambao umesaidia zaidi ya wagonjwa wenyeji kumi kurejesha uoni wao tangu mwaka jana,” amesema.

"Ghana inashukuru kwa walichokifanya," ofisa huyo amesisitiza.

Amesema kuwa wataalamu wote siyo tu wameongeza nguvu kazi katika hospitali hiyo lakini pia wametoa msaada wa vifaa tiba vinavyohitajika nchini Ghana, “Wema wao unapaswa kupongezwa."

Ofisa huyo ameliambia Xinhua kwamba anatazamia kuwakaribisha madaktari zaidi wa China nchini Ghana na ana imani watakuwa na jukumu kubwa la kutekeleza katika kukuza sekta ya afya nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Timu ya Madaktari wa China, katika Mwaka 2022 pekee, walipokea zaidi ya wagonjwa 13,000 wenyeji na kufanya upasuaji zaidi ya 800.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha