Kenya yapoteza mifugo milioni 2.61 kutokana na ukame

(CRI Online) Machi 03, 2023

Katika miezi kadhaa iliyopita, Kenya imepoteza mifugo ipatayo milioni 2.61 kutokana na ukame huku msukosuko huo ukiwa mbaya zaidi kwenye maeneo kame na nusu kame.

Kwenye ripoti yake iliyotolewa jana Alhamisi, Mamlaka ya Taifa ya Usimamazi wa Ukame ya Kenya (NDMA) imesema idadi hiyo inawakilisha asilimia ipatayo 5 ya mifugo yote inayofugwa katika maeneo kame na nusu kame, ambayo jumla yake inakadiriwa kufikia milioni 52.8.

Wanayama walioathirika zaidi na kufa kwa njaa katika kaunti mbili ambazo zimeathirika zaidi zikiwemo Marsabit na Kajiado, ni kondoo na ng'ombe. Ripoti hiyo imefafanua kuwa hali ya ukame imeendelea kuwa mbaya katika kaunti kame 22 kati ya 23, ikichangiwa na kunyesha kwa mvua chache katika Mwaka 2022 sanjari na kukosekana kwa mvua kwa misimu minne mfululizo.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, malisho katika maeneo kame yameisha kabisa, kutokana na joto kali. Hivi sasa serikali ya Kenya imetoa shilingi bilioni 2 (sawa na dola milioni 15.68 za Marekani) ili kuhakikisha usambazaji wa msaada wa chakula.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha