China kuwa na vituo vya msingi vya Teknolojia ya 5G milioni 2.9 kufikia mwisho wa Mwaka 2023

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 06, 2023

Waziri wa Viwanda na TEHAMA wa China Jin Zhuanglong akipokea mahojiano ya waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Bunge la Umma la 14 la China (NPC) mjini Beijing, China, Machi 5, 2023. (Xinhua/Cai Yang)

BEIJING - Waziri wa Viwanda na TEHAMA wa China Jin Zhuanglong amesema Jumapili kwamba China itakuwa imejenga zaidi ya vituo milioni 2.9 vya msingi vya teknolojia ya 5G ifikapo mwisho wa Mwaka 2023.

“Nchi inapanga kuongeza takriban vituo 600,000 kama hivyo mwaka huu, na kupanua wigo wa huduma za teknolojia za 5G katika maeneo ya vijijini na maeneo maalumu ya viwanda,” Jin amewaambia waandishi wa habari kando ya "mikutano miwili" inayoendelea.

China sasa ina zaidi ya vituo milioni 2.34 vya msingi vya teknolojia ya 5G, na idadi ya watumiaji wa simu za mkononi zenye kuunganishwa na teknolojia ya 5G imezidi milioni 575, amesema Waziri Jin, na kuongeza kuwa, teknolojia ya 5G inatumika sana katika uchumi, hasa katika uchimbaji wa madini, utoaji wa umeme na utengenezaji wa ndege kubwa za abiria.

Jin amesema juhudi zitafanywa katika kukuza matumizi ya viwandani ya teknolojia ya 5G, haswa katika utengenezaji bidhaa, na mipango ya kujenga zaidi ya viwanda 10,000 vinavyotumia teknolojia ya 5G katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Maendeleo ya Miaka Mitano (2021-2025).

“Utafiti na maendeleo ya teknolojia ya 6G pia yataharakishwa, kutokana na faida za soko kubwa la China na mfumo kamili wa viwanda,” amesema Jin.

"Mikutano miwili" ni mikutano miwili mikubwa ya kila mwaka ya Bunge la Umma la China, na Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Umma la China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha