Wakulima wanawake wapata faida kubwa kutokana na zao la tumbaku wakati msimu wa mnada unapoanza nchini Zimbabwe

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 13, 2023
Wakulima wanawake wapata faida kubwa kutokana na zao la tumbaku wakati msimu wa mnada unapoanza nchini Zimbabwe
Mwanamke akiendesha mkokoteni uliobeba marobota ya tumbaku kwenye Sakafu za Mnada wa Tumbaku huko Harare, Zimbabwe, Machi 9, 2023. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)

HARARE - Baada ya safari ndefu kutoka eneo la kilimo, Shylet Muzveba alikuwa akisubiri kwa shauku kubwa kwenye lori hapa ili kushusha marobota yake kwenye Sakafu za Mnada wa Tumbaku wa Harare, Zimbabwe.

Kisha akashusha pumzi ya ahueni baada ya kuwasili kwenye eneo maalum la kupakua mizigo. Amesema hivi karibuni atapata faida ya mavuno baada ya miezi kadhaa ya kuhangaika shambani.

Muzveba ni mmoja wa maelfu ya wakulima wadogo ambao wamechagua kulima na kukuza “jani la dhahabu” lenye malipo makubwa. Lakini kwa sasa, wasiwasi wake mkubwa ni bei ya kuuza, kwani hayuko chini ya kilimo cha mkataba, Muzveba ameliambia Shirika la Habari la Xinhua.

"Mwaka huu tumevuna mazao ya ubora wa juu. Tulipata mvua za kutosha, hivyo tunatarajia bei nzuri ili tuweze kununua pembejeo kwa msimu ujao," Muzveba amesema.

Tumbaku ni zao kuu la kuuzwa nje ya nchi linaloiingizia Zimbabwe mapato mengi zaidi na ni la pili kwa mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi baada ya dhahabu.

Kilo ya kwanza ya tumbaku kwa mwaka huu iliuzwa kwa dola za Kimarekani 4.35 ikilinganishwa na dola 4.20 mwaka jana.

Muzveba amesema anathamini zao hilo lenye faida kubwa baada ya kulima kwa miaka mitano.

"Nilikuwa nalima pamba na mahindi lakini niliacha ili niweze kujikita katika kulima tumbaku ambayo inaleta faida zaidi,"amesema.

Zimbabwe inakadiriwa kuzalisha kilo milioni 230 za tumbaku mwaka huu, kutoka kilo milioni 212 za mwaka jana kufuatia mvua nzuri na kuongezeka kwa hekta za ardhi iliyolimwa.

Nchi hiyo inalenga kuinua kiwango cha thamani ya nyongeza kutoka asilimia 2 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo Mwaka 2025, amesema Makamu wa Rais wa Zimbabwe Constantino Chiwenga Machi 8 wakati msimu wa uuzaji wa tumbaku kwa Mwaka 2023 ulipoanza.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha