China yazitaka nchi za Australia, Uingereza na Marekani (AUKUS) kutimiza kwa dhati wajibu wa kutoeneza Silaha za Nyuklia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 16, 2023

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin Jumatano amesema, China imezitaka Marekani, Uingereza na Australia ambazo kwa pamoja zinawakilishwa kwa kifupi kupitia ushirikiano wa AUKUS kutimiza kwa dhati wajibu wao wa kutoeneza silaha za nyuklia na kujiepusha kudhoofisha mamlaka na ufanisi wa mfumo wa usalama wa nyuklia wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa na vyombo vya habari, Machi 14, Marekani, Uingereza na Australia zilitangaza njia ya ushirikiano wa nyambizi za nyuklia. Nchi hizo tatu zilisema zimejitolea kuhakikisha viwango vya juu zaidi vya kutoeneza silaha za nyuklia vinafikiwa, na zitajadiliana na IAEA kuhusu mipango ya usalama wa nyuklia.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi amesema katika taarifa yake kwamba Shirika hilo litashauriana na Australia kufanya mpango chini ya Kifungu cha 14 cha Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa nyuklia wa Australia (CSA) kuhusiana na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT) ili kuwezesha Shirika hilo kufikia malengo yake ya usalama wa kiufundi wa nyuklia kwa Australia.

Wang amesema China inafuatilia kwa umakini zaidi kauli ya hivi karibuni ya Grossi kuhusu ushirikiano wa nyambizi za nyuklia wa AUKUS na inapinga vikali Marekani, Uingereza na Australia kuilazimisha Sekretarieti ya IAEA kuidhinisha masuala ya usalama wa nyuklia.

Wang amesema kwanza, nchi hizo tatu zilidai kuwa zitatimiza ahadi za kutoeneza silaha za nyuklia, lakini hii si chochote bali ni maneno tupu ya kuihadaa Dunia.

Msemaji huyo amesema pili, nchi za AUKUS na Sekretarieti ya IAEA hazina haki ya kufanya makubaliano kati yao kuhusu masuala ya usalama wa nyuklia kuhusiana na ushirikiano wa nyambizi za nyuklia wa AUKUS.

Wang amesema, kile ambacho nchi hizo tatu zinataka hasa ni msamaha wa IAEA wa usalama wa nyuklia kwa nyambizi za nyuklia za Australia, jambo ambalo linakwenda kinyume na walichosema kuhusu kuweka viwango vya juu zaidi vya kutosambaza silaha za nyuklia.

"Tatu, masuala ya usalama wa nyuklia yanayohusiana na ushirikiano wa nyambizi za nyuklia yanapaswa kujadiliwa kwa pamoja na kuamuliwa na jumuiya ya kimataifa,” Wang amesisitiza.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha