Rais Xi Jinping akutana na mwenzake Vladimir Putin huko Moscow

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 21, 2023

Rais wa China Xi Jinping akikutana na mwenzake wa Russia Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin baada ya kuwasili Moscow, Russia, Machi 20, 2023. (Xinhua/Shen Hong)

MOSCOW - Rais wa China Xi Jinping amekutana na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin, katika Ikulu ya Kremlin baada ya kuwasili Moscow siku ya Jumatatu.

Katika mazungumzo yao Rais Xi ameeleza kuwa amefurahi kufanya ziara nyingine ya kiserikali nchini Russia kwa mwaliko wa Putin, na Russia ilikuwa nchi ya kwanza aliyotembelea baada ya kuchaguliwa kwake kwa mara ya kwanza kuwa rais miaka 10 iliyopita na kumbukumbu kutoka kwenye ziara hiyo bado ni mpya leo.

Rais Xi amesisitiza kuwa kuna mantiki ya kihistoria ya uhusiano wa China na Russia kufikia hapa ulipo. Amesema, China na Russia ni jirani wakubwa na wenzi wa ushirikiano wa kimkakati kwa pande zote. Nchi zote mbili zinaona uhusiano wao kama kipaumbele cha juu katika diplomasia na sera zao za mambo ya nje.

Amesema China iko imara katika kufuata mwelekeo wa jumla wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Russia, na kuongeza kuwa China na Russia zimejitolea kufikia maendeleo na ustawishaji wa kitaifa, kuunga mkono Dunia yenye ncha nyingi na kufanyia kazi upanuzi zaidi wa demokrasia katika uhusiano wa kimataifa.

Rais Xi amesema nchi hizo mbili zinapaswa kuzidisha ushirikiano wa kivitendo katika sekta mbalimbali na kuimarisha uratibu na ushirikiano kwenye majukwaa ya uhusiano wa pande nyingi kama vile Umoja wa Mataifa ili kukuza maendeleo na ustawishaji wa mataifa yao, na kuwa ngome ya amani na utulivu duniani.

Kwa upande wake Putin amemkaribisha Rais Xi kwa ziara yake ya kiserikali nchini Russia na kwa mara nyingine tena amempongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa China.

Putin amesema katika miaka 10 iliyopita China imepata mafanikio ya kuvutia na makubwa katika sekta zote za maendeleo. Hii inatokana na uongozi bora wa Rais Xi na inathibitisha nguvu ya mfumo wa kitaifa wa kisiasa na mfumo wa utawala wa China.

Viongozi hao wawili pia wamebadilishana maoni kwa kina kuhusu suala la Ukraine.

Kuhusu hili, Rais Xi amesisitiza kuwa, sauti za amani na busara zinajengwa. Nchi nyingi zinaunga mkono kupunguza mvutano, kushikilia mazungumzo ya amani, na zinapinga kuongeza mafuta kwenye moto.

“China ilitoa waraka kuhusu msimamo wake kuhusu msukosuko wa Ukraine, ikitetea utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo na kukataa mawazo ya Vita Baridi na vikwazo vya upande mmoja,” amesema Xi. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha