Idara ya Forodha ya China yasema Biashara ya nje ya China imeanza vizuri Mwaka 2023

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 21, 2023

Picha hii iliyopigwa Tarehe 13 Machi 2023 ikionyesha kituo cha kontena cha Bandari ya Taicang, Mkoa wa Jiangsu nchini China. (Xinhua/Li Bo)

BEIJING - Biashara ya nje ya China imeanza vyema mwaka huu, ikiwa na mwelekeo mzuri unaotarajiwa kufuata baadaye, Yu Jianhua, Mkuu wa Idara ya Forodha ya China (GAC) amesema.

“Idadi ya makontena ya kusafirishwa nje ya nchi imekuwa ikiongezeka tangu mwishoni mwa Februari,” Yu ameuambia mkutano na waandishi wa habari, wakati akifafanua kuhusu tetesi za hivi karibuni za uwepo wa makontena matupu yaliyorundikwa kwenye bandari za China hali ambayo imezua wasiwasi juu ya biashara ya nchi hiyo.

Amesema kuwa, takwimu za kila wiki za idara hiyo zinaonyesha kuwa biashara imekuwa ikiimarika kuanzia mwezi Februari. Ingawa biashara ya nje ya bidhaa ilipungua kwa asilimia 0.8 kuliko ile ya mwaka jana katika miezi miwili ya kwanza, mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 0.9 ikiwa ni kwa kiwango bora zaidi kuliko ilivyotarajiwa.

“Kampuni za biashara zimeripoti kuongezeka kwa idadi ya oda mpya, na jumla ya mauzo ya nje ya magari yanayotumia nishati ya umeme, betri za lithiamu-ioni na betri za jua yaliongezeka katika miezi miwili ya kwanza,” Yu amesema. “Mambo muhimu haya yanaweza kuimarisha ukuaji wa biashara katika miezi ijayo,” ameongeza.

Hata hivyo, Yu ameonya dhidi ya changamoto zinazowezekana kama vile kufifia kwa mahitaji ya nje na malipo ya polepole kutoka kwa baadhi ya nchi. Shirika la Biashara Duniani (WTO) lilipunguza makadirio yake ya ukuaji wa biashara ya kimataifa kwa Mwaka 2023 kutoka asilimia 3.4 hadi asilimia 1 Mwezi Oktoba mwaka jana.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha