Kenya yaongeza ufuatiliaji baada ya mlipuko wa virusi vya Marburg kuibuka Tanzania

(CRI Online) Machi 24, 2023

Wizara ya Afya ya Kenya imesema ipo kwenye tahadhari kubwa baada ya jirani yake Tanzania kugundua mgonjwa wa kwanza wa virusi vya ugonjwa wa Marburg katika Mkoa wa Kagera, ambapo imewaelekeza wafanyakazi wote wa afya katika vituo mbalimbali vya mipakani kuhakikisha wasafiri wote wanaotoka Tanzania na kuingia Kenya wanachunguzwa.

Jumanne Wizara ya Afya ya Tanzania ilisema kuwa vipimo vya maabara vinaonesha kuwa ugonjwa wa ajabu ambao umeua watu watano mkoani Kagera wiki iliyopita ulisababishwa na virusi vya Marburg.

Benjamin Murkomen, afisa wa afya wa mipakani katika Wizara ya Afya ya Kenya, amewaelekeza wafanyakazi wote wanaofuatilia afya za watu na timu za kukabiliana na matukio ya dharura kuimarisha uchunguzi wakati virusi vinaendelea kuenea baadhi ya sehemu za Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Matshidiso Moeti amesema Shirika hilo linashirikiana na serikali ya Tanzania kuongeza kasi ya hatua za kudhibiti ili kuzuia kuenea kwa virusi na kumaliza mlipuko huo haraka iwezekanavyo.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha