Kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na China kwapongezwa kote Honduras

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 28, 2023

Picha hii iliyopigwa Tarehe 26 Machi 2023 ikionyesha mandhari ya Tegucigalpa, Mji Mkuu wa Nchi ya Honduras. (Xinhua/Xin Yuewei)

TEGUCIGALPA - Watu kutoka sekta mbalimbali nchini Honduras wamepongeza kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Honduras baada ya nchi hizo mbili kutia saini taarifa ya pamoja Jumapili iliyopita.

Rodolfo Pastor de Maria, Katibu wa Ofisi ya Rais wa Honduras ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa ni heshima kubwa kushuhudia kuanzishwa kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, jambo ambalo litafungua mlango muhimu wa fursa kwa Honduras na kuisaidia nchi hiyo kubadilisha uhusiano wake wa kimataifa.

“Kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Honduras ni uamuzi wa kihistoria uliofanywa kwa kujitegemea na kwa ujasiri, na hakuna nchi inayoweza kupuuza hadhi na nafasi ya China kama nchi kubwa katika masuala ya uchumi, fedha na biashara,” Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Honduras, Manuel Antonio Diaz amesema.

Waziri wa Elimu wa Honduras Daniel Sponda amesema, Uchumi wa China umepata ukuaji thabiti, na bidhaa zinazotengenezwa nchini China zimesafirishwa duniani kote, na kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na China kutasaidia Honduras kupata maendeleo ya ujuzi wa kidijitali katika elimu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Forodha ya Honduras, Fausto Calix, amesema kuwa Honduras ikiwa nchi yenye mamlaka imefanya uamuzi huo, na lazima uamuzi huo uheshimiwe na jumuiya ya kimataifa, na China ikiwa nchi kubwa duniani, italeta fursa kubwa kwa maendeleo ya nchi ya Honduras.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha