IGAD yaomba dola bilioni 2.7 kusaidia waathiriwa wa ukame katika Pembe ya Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 29, 2023

Picha ya kumbukumbu ikimwonyesha mwanakijiji Caroline akiwa amesimama kwenye shamba la mahindi lililoathiriwa na ukame katika eneo dogo la Kidemu lililoko Kaunti ya Kilifi, Kenya, Tarehe 23 Machi 2022. (Xinhua/Dong Jianghui)

NAIROBI - Shirika la Kiserikali la Maendeleo la Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) Jumatatu lilitangaza kuomba ufadhili wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2.69 ili kuokoa mamilioni ya watu walio katika hatari ya njaa kutokana na ukame katika nchi za Kenya, Ethiopia na Somalia.

Katibu Mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu amesema hali inaendelea kuwa mbaya zaidi, huku watu milioni 47 wakiwa na hali ya ukosefu wa usalama wa chakula na wengine wako katika hatari ya kufa kwa njaa.

"Asilimia 70 ya watu hawa milioni 47 wanaishi Ethiopia, Kenya, na Somalia," amesema katika taarifa iliyotolewa Nairobi, Kenya. "Hii ndiyo sababu leo, tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutusaidia kuzuia maafa makubwa ya kibinadamu kwa kutoa rasilimali zinazohitajika kuokoa maisha na shughuli za watu kwa muda mfupi, na kuendelea kuwekeza katika kujenga uhimilivu katika muda wa kati na mrefu."

Kwa mujibu wa shirika hilo, Somalia inahitaji dola bilioni 1.6 ili kutoa msaada wa chakula na bidhaa zisizo za chakula kwa jamii zilizoathiriwa na ukame na wakimbizi wa ndani; Ethiopia inahitaji dola milioni 710 ili kutoa msaada kwa mahitaji muhimu ya kisekta katika miezi minne ijayo; na Kenya inahitaji dola milioni 378 ili kutoa msaada wa chakula, maji na chanjo kwa kaunti zilizoathiriwa hadi kufikia Oktoba.

IGAD imesema ukame umesababisha madhara mabaya, ikiwa ni pamoja na uhaba mkubwa wa maji na malisho, watu milioni moja kuyakimbia makazi, na vifo vya mifugo na wanyamapori vimefikia zaidi ya milioni 10, na kupungua kwa uzalishaji wa mazao na mifugo, ambayo yote yanaongeza hali ya ukosefu wa usalama wa chakula.

Picha ya kumbukumbu ikionyesha familia ikipata mlo katika Wilaya ya Baidoa, Somalia, Januari 20, 2023. (Picha na Abdi/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha