Waziri Mkuu wa China akutana na Mkurugenzi Mkuu wa IMF huko Boao, Hainan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 30, 2023

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Kristalina Georgieva, ambaye anahudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia 2023, huko Boao, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 29, 2023. (Xinhua/Liu Bin)

BOAO, Hainan - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Kristalina Georgieva Jumatano huko Boao, Mkoa wa Hainan, nchini China huku akiahidi kuimarisha ushirikiano na IMF ili kufanya usimamizi wa dunia kuwa wenye haki na usawa zaidi.

Waziri Mkuu Li amesema, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, uchumi wa China umeonyesha kasi ya kuimarika na kufufuka, China ina msingi imara wa uchumi, matarajio mapana ya maendeleo na mustakabali wenye matumaini. Amesema, China itaimarisha udhibiti wa sera za uchumi mkuu, kuongeza nguvu kwenye matumizi nchini na uwekezaji, kufungua mlango kwa Dunia bila kuyumbayumba, kuboresha kwa pande zote mazingira ya biashara, na kuzuia na kupunguza hatari kwa uangalifu.

"Tuna imani na uwezo wa kukuza uboreshaji wa uchumi kwa ujumla na kufikia malengo ya maendeleo ya mwaka mzima," amesema.

Katika kukabiliana na changamoto ngumu na kali, jumuiya ya kimataifa inahitaji kushirikiana kwa pamoja ili kukabiliana nazo, Waziri Mkuu Li amesema, huku akiitaka jumuiya ya kimataifa kudumisha ushirikiano wa pande nyingi, kuimarisha uratibu wa sera za uchumi mkuu, na kudumisha usalama, utulivu na urahisi wa minyororo ya viwanda ya dunia nzima.

Amesema China inatilia maanani sana uhusiano wake na IMF, inaunga mkono kwa dhati IMF katika kutekeleza jukumu muhimu katika usimamizi wa dunia, na iko tayari kuimarisha ushirikiano na IMF ili kufanya usimamizi wa dunia uwe wenye haki na usawa na kuongeza sauti na ushawishi wa masoko yanayoibukia, na nchi zinazoendelea katika masuala ya kimataifa.

Kwa upande mkuu huyo wa IMF, Georgieva ambaye yuko China kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Boao la Asia 2023, ameeleza kuwa China ni mshirika mwenzi muhimu wa IMF, maendeleo ya uchumi wa China yana kasi nzuri na yanatarajiwa kuchangia zaidi ya theluthi moja ya ukuaji wa uchumi wa Dunia mwaka huu, jambo ambalo litatoa fursa muhimu kwa nchi nyingine. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha