Mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa atoa wito kwa makundi yenye silaha nchini DRC kukomesha ghasia zote

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 31, 2023

UMOJA WA MATAIFA- Kaimu Mjumbe wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Dai Bing Jumatano ametoa wito kwa makundi yenye silaha Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kukomesha vitendo vyao vyote vya ghasia na kuondoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Amesema kwenye mkutano wa majumuisho wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, kuendelea kwa mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha Mashariki mwa DRC kunaweza kuifanya hali ya usalama nchini humo izidi kuwa mbaya katika wakati serikali ya DRC inapofanya juhudi za dhati za kuendeleza mageuzi ya sekta ya usalama, kupambana na makundi yenye silaha, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu.

"Kusitisha mapigano na kukomesha ghasia ni vipaumbele vya juu," amesema.

Dai ameeleza kuwa kwa msaada wa Umoja wa Afrika na nchi za kikanda kama vile Angola, Kundi la waasi la M23 lilikubali kusitisha mapigano na kushiriki kwenye mazungumzo mapema mwezi wa Machi mwaka huu.

Mjumbe huyo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono kwa nguvu jitihada za kutoa misaada ya kibinadamu, huku akizungumzia "mahitaji makubwa ya kibinadamu" Mashariki mwa DRC kutokana na hali mbaya zaidi.

“Mashirika husika ya Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC wanapaswa kufanya kazi pamoja ili kutumia kikamilifu ufanisi wa makadirio yake ya hali ya ubinadamu na kuhakikisha utoaji wa mahitaji muhimu ulio salama na rahisi” amesema.

Amesema China iko tayari kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa kutoa mchango zaidi kwa ajili ya amani na maendeleo ya DRC.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha