

Lugha Nyingine
Tanzania yapanga mpango wa kuajiri wahudumu wa afya na walimu 21,000 ili kupunguza tatizo la upungufu
DAR ES SALAAM - Serikali ya Tanzania Jumatano imetangaza nafasi za kazi kwa watumishi wa afya na walimu 21,200 kwa lengo la kutatua tatizo lililopo la upungufu wa wafanyakazi katika sekta ya afya na elimu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Tanzania Angellah Kairuki amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kuajiriwa kwa watumishi wapya wa afya na walimu.
Kairuki ameuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa chini ya utaratibu huo, walimu 13,130 wa shule za msingi wataajiriwa ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa walimu linalozikabili shule za msingi za umma kote nchini Tanzania.
Pia amesema wahudumu wa afya 8,070 wataajiriwa na kutumwa katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati kote nchini humo ambazo zinahitaji wahudumu wa afya.
"Mchakato wa ajira umefunguliwa Jumatano na utafungwa Aprili 25,” amesema Kairuki, na kuongeza kuwa hatua za adhabu zitachukuliwa dhidi ya maofisa ambao watahusishwa na utovu wowote wa taratibu za uajiri katika mchakato wa kuajiri.
Kairuki amesema Watanzania wenye sifa wanaweza kutuma maombi kupitia tovuti ya wizara ya ajira, na waombaji wawe ni wale tu waliohitimu katika vyuo vinavyotambuliwa na Serikali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma