

Lugha Nyingine
China iko tayari kuwezesha kuanza tena kwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina
Beijing - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang amesema hapa Jumatatu kuwa, China inazihimiza Israeli na Palestina kuonyesha ujasiri wa kisiasa na kuchukua hatua za kuanza tena mazungumzo ya amani, na China iko tayari kuweka mazingira rahisi na wezeshi ya kufanyika kwa hili.
Katika mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen, Qin Gang amesema China ina wasiwasi na mvutano uliopo kati ya Israel na Palestina, na kipaumbele cha sasa cha juu ni kudhibiti hali na kuzuia mgogoro huo usizidi kuwa mbaya au hata kutoka nje ya udhibiti.
Qin Gang amesema, Pande zote zinapaswa kudumisha utulivu na kujizuia, na kuacha kauli na vitendo vya kupindukia kiasi na vya kichochezi, na njia ya msingi ni kuanzisha tena mazungumzo ya amani na kutekeleza "suluhu ya nchi mbili."
“Haijachelewa sana kufanya jambo sahihi,” amesema.
Qin amesema Rais wa China Xi Jinping ameweka mbele Pendekezo la Usalama wa Dunia, na China inaamini kwamba ufunguo wa kutatua suala la Israeli na Palestina upo katika kutilia maanani maono ya usalama wa pamoja.
Amesema China haina maslahi binafsi katika suala la Israel na Palestina, na inatumai kuwa Israel na Palestina zinaweza kuishi pamoja kwa amani na kulinda amani na utulivu wa kikanda.
Qin amesema, China iko tayari kuimarisha mawasiliano katika ngazi zote na Israel, kuongeza kuaminiana kisiasa na kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana.
Kwa upande wake Cohen ameishukuru China kwa nia yake ya kuunga mkono suluhu ya mgogoro wa Israel na Palestina. Amesema, Israel imejitolea kutuliza hali hiyo, lakini tatizo hilo halina uwezekano wa kutatuliwa kwa muda mfupi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma