

Lugha Nyingine
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres atoa wito wa kufanya mazungumzo kutatua mgogoro nchini Sudan
Picha hii iliyopigwa Tarehe 15 Aprili 2023 ikionyesha moshi ukifuka Khartoum, Sudan. (Picha na Mohamed Khidir/Xinhua)
UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka viongozi wa Vikosi vya Jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan kusitisha mara moja uhasama na kuanza mazungumzo ya kutatua mgogoro wa Sudan.
Guterres ametoa wito huo kabla ya kutoa hotuba yake ya ufunguzi kwenye kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu ufadhili wa maendeleo.
Amelaani vikali kuzuka kwa mapigano nchini Sudan, akieleza kuwa hali hiyo tayari imesababisha "matukio mabaya ya kupoteza maisha" vikiwemo vifo vya raia wengi.
Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano ya kutumia silaha kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya nchi hiyo tokea Aprili 15.
Takriban watu 97 wameuawa na mamia wengine kujeruhiwa tangu kuanza kwa mapigano hayo, kwa mujibu wa Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan, shirika lisilo la kiserikali.
"Ninalaani matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa raia na wafanyakazi wa kibinadamu na kulengwa na uporaji wa kwenye majengo," amesema Guterres.
"Nazikumbusha pande zote juu ya haja ya kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wa wafanyakazi na wote wanaohusika wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu."
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba kuendelea kuchochea kwa aina yoyote kunaweza kuleta matokeo mabaya kwa Sudan na kanda hiyo, na kuwataka wale wote wenye ushawishi juu ya hali hiyo kuunga mkono juhudi za kukomesha ghasia, kurejesha utulivu, na kurejea kwenye njia ya mpito.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Tafakari ya Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi ya Mwaka 1994 nchini Rwanda kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Aprili 14, 2023. (Loey Felipe/Picha/ Umoja wa Mataifa/Xinhua )
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma