Katibu Mkuu wa UN asema mgogoro wa Sudan unaweza kuathiri kanda na maeneo mengine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 25, 2023

Picha hii iliyopigwa Aprili 19, 2023 ikionyesha duka lililofungwa huko Khartoum, Sudan. (Picha na Mohamed Khidir/Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Aprili 19, 2023 ikionyesha duka lililofungwa huko Khartoum, Sudan. (Picha na Mohamed Khidir/Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya Jumatatu kwamba mgogoro wa kijeshi nchini Sudan unaweza kukumba kanda nzima pamoja na maeneo mengine.

Amesema, hali nchini Sudan inaendelea kuwa mbaya. Tangu kuanza kwa mapigano Aprili 15, mamia ya watu wameuawa na maelfu wengine kujeruhiwa.

"Vurugu lazima zikome. Inahatarisha kuleta moto wa hatari ndani ya Sudan ambao unaweza kukumba kanda yote na kwingineko," ameonya.

Guterres ametoa tahadhari hiyo mwanzoni mwa hotuba yake kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uhusiano wa pande nyingi.

"Nalaani vikali upigaji mabomu usiochagua katika maeneo ya kiraia vikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya. Natoa wito kwa wahusika kusitisha oparesheni za kivita katika maeneo yenye msongamano wa watu na kuruhusu shughuli za misaada ya kibinadamu bila vikwazo. Raia lazima waweze kupata chakula, maji na vifaa vingine muhimu, na kuondoka kutoka maeneo ya mapigano," Guterres amesema.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na pande zinazohusika katika mgogoro huo na ametoa wito kwao kupunguza mvutano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

“Umoja wa Mataifa utaendelea na juhudi zake na washirika ili kufanikisha kufikia usitishaji wa kudumu wa mapigano haraka iwezekanavyo,” ameongeza.

Mapigano makali yalizuka kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka mnamo Aprili 15 katika Mji Mkuu, Khartoum na maeneo mengine, na kufifisha matumaini ya kurejea kwa utawala wa kiraia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wito wa kusimamisha mapigano kwa siku tatu nchini Sudan kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Aprili 20, 2023. (Xinhua/Xie E)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wito wa kusimamisha mapigano kwa siku tatu nchini Sudan kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Aprili 20, 2023. (Xinhua/Xie E)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha