

Lugha Nyingine
Rais Biden azindua rasmi kampeni ya kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa Mwaka 2024
Rais wa Marekani Joe Biden akitoa hotuba kwenye hafla katika Ikulu ya Marekani huko Washington, D.C., Marekani, Aprili 24, 2023. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua)
WASHINGTON - Rais wa Marekani Joe Biden amezindua rasmi kampeni yake ya kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani wa Mwaka 2024 siku ya Jumanne.
"Nilipogombea urais miaka minne iliyopita, nilisema tuko kwenye mapambano kwa ajili ya roho ya Marekani. Na bado tupo kwenye mapambano hayo," Biden, mwanachama wa Chama cha Democrat amesema katika video iliyotolewa mapema asubuhi.
Tangazo hilo lilitolewa siku ya kumbukumbu ya miaka minne ya Biden kuzindua kampeni yake ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020 wa Marekani.
Julie Chavez Rodriguez, Afisa Mwandamizi wa Ikulu ya White House na mwanaharakati wa muda mrefu wa Chama cha Democrat, anatarajiwa kusimamia kampeni ya uchaguzi ya Biden ya Mwaka 2024.
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump -- ambaye alishindwa na Biden kwenye uchaguzi wa Mwaka 2020 lakini ameendelea kukataa kushindwa – ni muongozaji wa mapema wa kugombea nafasi ya urais kupitia uteuzi wa Chama cha Republican wa Mwaka 2024.
Trump alimshambulia Biden katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, na kuuita urais wake kuwa ni "janga na umeshindwa."
Uchaguzi wa urais wa Marekani wa Mwaka 2024 umepangwa kufanyika Novemba 5, 2024.
Kwa mujibu wa kura mpya ya maoni ya kitaifa ya Kituo cha Habari cha NBC, hakuna hamu kubwa ya umma wa Marekani kwa marudio ya mpambano wa kati ya Biden na Trump katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Kura hiyo ya maoni inaonesha kuwa, asilimia 70 ya Wamarekani wote, ikiwa ni pamoja na asilimia 51 ya wanachama wa Chama cha Democrat, wanadhani kwamba Biden hapaswi kugombea muhula wa pili. Nusu ya wale wanaosema Biden, mwenye umri wa miaka 80, hapaswi kugombea tena wanataja umri wake kama sababu "kuu".
Kuhusu Trump, kura hiyo ya maoni inasema asilimia 60 ya Wamarekani, ikiwa ni pamoja na theluthi moja ya wanachama wa Chama cha Republican, wanaamini kwamba hapaswi kugombea Mwaka 2024.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma