

Lugha Nyingine
Usimamishaji Mapigano kwa saa 72 waanza nchini Sudan huku kukiwa na milio ya risasi mjini Khartoum
Watu waliohamishwa kutoka Sudan wakiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Marka mjini Amman, Jordan, Aprili 24, 2023. (Xinhua/Mohammad Abu Ghosh)
KHARTOUM - Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vimetangaza Jumanne kwamba mapatano mapya ya kusimamisha mapigano kwa saa 72 yameanza kutekelezwa, licha ya kuendelea kusikika kwa milio ya risasi mjini Khartoum na pande hizo mbili zinazopigana zinashutumu kila mmoja kwa ukiukaji wa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Jeshi la Sudan, jeshi hilo limesema limekubali makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa saa 72 yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia kwa malengo ya kibinadamu, na kwa masharti kwamba "waasi wajitolee kusitisha mapigano yote na kutii masharti ya kuendelea kwake."
RSF ilitangaza katika taarifa yake kwamba "imekubali makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa saa 72 ili kufungua njia za kibinadamu, kuwezesha matembezi ya raia na wakaazi kwa ajili ya kuwawezesha kupata mahitaji yao, kufika hospitalini na maeneo salama, na kuhamisha wajumbe wa kidiplomasia."
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza katika taarifa yake kwamba makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo makali katika kipindi cha muda wa saa 48 zilizopita, na kuzitaka pande zote mbili "kuunga mkono mara moja na kikamilifu usimamishaji vita."
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken makubaliano hayo yalianza saa sita usiku Aprili 24 na yatadumu kwa saa 72.
Hata hivyo saa chache baadaye pande hizo mbili zilianza kulaumiana kwa kukiuka makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, huku walioshuhudia wakisema milio ya risasi ilisikika katika maeneo mbalimbali kote Khartoum, hasa katika mtaa wa Omdurman.
Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali ya silaha kati ya Jeshi la Sudan na RSF mjini Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15. Pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kuanzisha mgogoro huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kuhusu Sudan kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano wa pande nyingi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Aprili 24, 2023. Guterres ameonya kwamba mgogoro wa kijeshi nchini Sudan unaweza kuenea kanda nzima na maeneo mengine. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma