

Lugha Nyingine
Uturuki yatoa nishani za serikali kwa vikosi vya uokoaji vya ndani na nje ya nchi kwa juhudi zao za uokoaji wakati wa tetemeko
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (wa kwanza kushoto, mbele) na Wang Mo (wa pili kushoto, mbele), Naibu Mkuu wa Kikosi cha Uokoaji cha China, wakihudhuria hafla ya kukabidhi nishani za serikali mjini Ankara, Uturuki, Aprili 25, 2023. Erdogan siku ya Jumanne ilitoa nishani za serikali kwa wafanyakazi 55,000 kutoka vikosi vya uokoaji vya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuthamini michango yao katika juhudi za uokoaji na utoaji misaada baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea Mwezi Februari mwaka huu. (Picha na Mustafa Kaya/Xinhua)
ANKARA - Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumanne alitoa nishani za serikali kwa wafanyakazi 55,000 kutoka vikosi vya uokoaji vya ndani na nje ya nchi hiyo kwa lengo la kuthamini michango yao katika juhudi za uokoaji na utoaji wa misaada baada ya matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea Mwezi Februari mwaka huu.
"Leo, tutawasilisha nishani kwa vikosi vya utafutaji na uokoaji vya ndani na nje ya nchi ambavyo vilijitolea mhanga wakati wa tetemeko la Februari 6," Erdogan amesema kwenye hafla ya uwasilishaji iliyofanyika katika Mji Mkuu, Ankara.
Erdogan amesema wafanyakazi 11,320 kutoka nchi 90 walikwenda Uturuki kujiunga na juhudi za uokoaji na utoaji misaada kutokana na matetemeko hayo, na nchi na mashirika ya kimataifa 60 yalituma karibu mahema 250,000 nchini Uturuki.
Matetemeko hayo makubwa, ambayo yalitikisa Kusini mwa Uturuki mnamo Februari 6, yamesababisha watu zaidi ya 50,000 kupoteza maisha, na kuharibu maelfu ya majengo na kuwaacha makumi kwa maelfu ya watu bila makazi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma