Waziri Mkuu wa China Li Qiang akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki ya Ubunifu Duniani (WIPO) mjini Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 28, 2023

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki ya Ubunifu Duniani (WIPO) Daren Tang mjini Beijing, China, Aprili 27, 2023. (Xinhua/Liu Weibing)

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki ya Ubunifu Duniani (WIPO) Daren Tang mjini Beijing, China, Aprili 27, 2023. (Xinhua/Liu Weibing)

BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki ya Ubunifu Duniani (WIPO) Daren Tang siku ya Alhamisi mjini Beijing.

Akieleza kuwa mwaka huu ni Maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano kati ya China na WIPO, Waziri Mkuu Li amesema Rais wa China Xi Jinping ametuma barua ya pongezi kwa maadhimisho hayo, na China inatarajia kutumia fursa hiyo kusukuma ushirikiano kuelekea kwenye ngazi mpya.

Waziri Mkuu Li amesema China siku zote inatilia maanani kulinda hakimiliki ya ubunifu, kutekeleza mkakati wa kitaifa wa hakimiliki ya ubunifu, na kufanya juhudi za kuifanya nchi ya China kuwa na nguvu kwenye mambo ya hakimiliki ya ubunifu.

Amesema China imepata mafanikio makubwa katika kuanzisha na kuimarisha ulinzi wa kisheria wa hakimiliki ya ubunifu, kukamilisha utaratibu wa usimamizi wa IPR, kuongeza uelewa wa jamii nzima kuhusu kuheshimu na kulinda hakimiliki ya ubunifu, na kushughulikia kesi kubwa za kukiuka hakimiliki ya ubunifu kwa mujibu wa sheria.

Waziri Mkuu Li amesema kuwa China ni mjengaji mwenye hamasa kubwa, mchangiaji muhimu na mtetezi shupavu wa utaratibu wa kimataifa wa hakimiliki ya ubunifu.

Akisisitiza umuhimu wa hakimiliki ya ubunifu, Waziri Mkuu Li amesema kuwa kazi ya hakimiliki ya ubunifu inakabiliwa na matatizo mengi mapya na changamoto katika wakati wa kupatikana kwa maendeleo ya teknolojia za akili bandia, Mtandao wa Mambo na teknolojia nyingine mpya, pamoja na uchumi wa kidijitali.

Waziri Mkuu Li amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano na WIPO, ili kutoa mchango kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri yanayosaidia uvumbuzi, ulinzi na matumizi ya hakimiliki ya ubunifu.

Kwa upande wake Tang amepongeza mafanikio ya kihistoria na maendeleo ambayo China imepata kuhusu hakimiliki ya ubunifu katika miaka 50 iliyopita.

“Mkakati wa hakimiliki ya ubunifu wa China ni wa kupigiwa mfano,” amesema Tang na kuongeza kuwa WIPO ina ushirikiano mkubwa na China kwa pande zote katika nyanja za uvumbuzi, teknolojia na uwekaji mifumo ya kidijitali.

Tang amesema WIPO itaimarisha zaidi ushirikiano na China siku zijazo ili kukuza maendeleo ya ubunifu ya Dunia na maendeleo ya nchi zote kwa pamoja. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha