Russia yasema Ukraine imejaribu kuishambulia Ikulu ya Kremlin kwa kutumia droni huku Kiev ikikana kuhusika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 04, 2023

Bendera ya Taifa la Russia ikipepea katika Ikulu ya Kremlin mjini Moscow, Russia, Januari 6, 2023. (Picha na Alexander Zemlianichenko Jr/Xinhua)

Bendera ya Taifa la Russia ikipepea katika Ikulu ya Kremlin mjini Moscow, Russia, Januari 6, 2023. (Picha na Alexander Zemlianichenko Jr/Xinhua)

MOSCOW/KIEV - Ofisi ya habari ya Ikulu ya Russia imesema Jumatano kwamba, Ukraine imejaribu kumuua Rais wa Russia Vladimir Putin Jumanne usiku kwa kutumia droni mbili kushambulia makazi yake ya Kremlin.

Ikulu ya Kremlin imesema jeshi na vikosi maalum vilitumia rada za kivita kuzima droni hizo.

Imesema, licha ya jaribio la shambulizi hilo, hakuna majeruhi au uharibifu wa mali ulioripotiwa kutoka kwenye udondoshaji wa droni hizo na vipande vilivyotawanyika baada ya kudondoshwa.

"Tunachukulia hatua hiyo kama kitendo cha kigaidi kilichopangwa na jaribio la kukatisha maisha ya Rais wa Russia, ambalo limefanyika usiku wa kuamkia Gwaride la Siku ya kumbukumbu ya Ushindi ya Mei 9, ambapo wageni kutoka nje ya nchi wanapanga kuhudhuria," Kremlin imesema.

Kwa mujibu wa msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, Rais Putin hakuwa Kremlin wakati wa shambulio hilo na alikuwa akifanya kazi katika makazi ya rais ya Novo-Ogaryovo katika kitongoji cha Moscow siku ya Jumatano.

Mshauri wa Rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak ameliambia Ukrinform, Shirika la Habari la Ukraine linalosimamiwa na serikali kwamba Ukraine haihusiki katika shambulio hilo la droni dhidi ya Kremlin.

"Ukraine haikushambulia Kremlin au vituo vyovyote kwenye eneo la Shirikisho la Russia," Podolyak amesema, akibainisha kuwa vikosi vya kijeshi vya Ukraine vinalenga vituo vya kijeshi pekee katika maeneo yaliyokaliwa kwa muda ya Ukraine.

Amefafanua kuwa mashambulizi dhidi ya vituo nchini Russia, ikiwa ni pamoja na Kremlin, hayatoi mchango kwa madhumuni yoyote ya kijeshi au kuchangia katika maandalizi ya Ukraine kwa ajili ya operesheni yoyote ya mashambulizi ya kujibu.

Meya wa Moscow Sergei Sobyanin ametangaza siku ya Jumatano kupiga marufuku kurusha droni katika mji mkuu huo wa Russia. Kremlin imesema Russia inahifadhi haki ya kujibu ipasavyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha