China yashinda Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Msururu ya 2023 FIBA 3x3 kwa wanawake huko Wuhan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2023
China yashinda Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Msururu ya 2023 FIBA 3x3 kwa wanawake huko Wuhan
Wachezaji wa China wakipiga picha baada ya kushinda taji la Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Msururu ya 2023 FIBA 3x3 kwa wanawake mjini Wuhan, China mnamo Mei 7, 2023. (Xinhua/Xiao Yijiu)

WUHAN - China imetwaa taji katika kituo cha kwanza cha Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Msururu ya 2023 FIBA ya wachezaji watatu dhidi ya watatu (3x3) kwa wanawake baada ya kuichapa Australia jumla ya pointi za vikapu 21 kwa 13 hapa Jumapili.

China na Australia zote hazikuruhusu kufungwa katika mbio zao kabla ya kufikia fainali. Mbele ya umati wa watu wa nyumbani, China iliingia kwenye mchezo haraka na kupanua uongozi wake wakati mechi ikiendelea, huku Zhang Zhiting akifunga vikapu mfululizo kujipatia ushindi wake.

"Ilikuwa fursa muhimu kwetu kuifanyia majaribio timu yetu kabla ya Kombe la Dunia. Wachezaji wetu walifanya kazi kwa bidii wakati wote wa mashindano haya," amesema kocha mkuu wa China Xu Jiamin.

Timu ya China kwa mfululizo wa mashindano haya inahusisha washindi wa medali ya shaba kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Wang Lili, Zhang Zhiting na Wan Jiyuan, pamoja na Zhang Yi, ambaye amesajiliwa katika timu hiyo mwaka huu.

Zhang Zhiting alifunga vikapu vingi zaidi katika mchezo huo kwa kufikisha pointi tisa. Wang, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora (MVP) wa mashindano hayo, alikuwa na pointi tatu, huku Wan na Zhang Yi wakichangia pointi tano na nne mtawalia.

"Inahisi tofauti kabisa kucheza pamoja na wachezaji wazoefu kwani nina amani ya akili na ninaweza kujionesha kikamilifu kwenye uwanja," amesema Zhang Yi.

Timu ya China itarudi Beijing siku ya Jumatatu, na kupanga kushindana katika kituo kijacho cha Msururu wa Astara, Azerbaijan baada ya kipindi kifupi cha mapumziko.

Kombe la Dunia la FIBA 3x3 litafanyika Vienna, Austria kuanzia Mei 30 hadi Juni 4.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha