Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yaunda tume ya mawaziri kushughulikia mgogoro wa Sudan

(CRI Online) Mei 08, 2023

Baraza la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu limetoa azimio jana Jumapili la kuunda tume ya mawasiliano ya mawaziri wa nchi za Kiarabu ili kuwasiliana na pande mbalimbali za Sudan na nchi zenye ushawishi za kikanda na kimataifa pamoja na mashirika husika ya kimataifa, kwa lengo la kufikia suluhu ya mgogoro wa Sudan.

Azimio hilo lililotolewa kwenye mkutano maalumu wa Baraza hilo uliofanyika Cairo nchini Misri, linalenga kuzidisha juhudi za nchi za Kiarabu kutafuta suluhu ya amani kwenye mgogoro uliopo nchini Sudan kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao ulizuka katikati ya mwezi Aprili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, chini ya azimio hilo, tume hiyo ya mawasiliano itajumuisha wawakilishi kutoka Saudi Arabia, Misri, na Jumuiya ya Kiarabu. Tume hiyo inalenga kufikia usitishaji vita kamili na endelevu nchini Sudan na kushughulikia sababu za mgogoro huo.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha