Mji wa Dalian nchini China waanzisha njia mpya ya kusafirisha makontena kupitia baharini hadi Ulaya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 10, 2023
Mji wa Dalian nchini China waanzisha njia mpya ya kusafirisha makontena kupitia baharini hadi Ulaya
Meli ya kubeba makontena ya MSC Katie ikiwa tayari kuondoka kwenye Kituo cha Kontena cha Dalian huko Dalian, Mkoa wa Liaoning, Kaskazini-Mashariki mwa China, Mei 8, 2023. (Xinhua/Guo Xiang)

DALIAN – Meli ya kubeba makontena ya MSC Katie imeondoka kwenye Kituo cha Kontena cha Dalian katika Mji wa Dalian ulioko Mkoa wa Liaoning wa China siku ya Jumatatu, kuelekea pwani ya magharibi ya Bahari ya Mediterania. Safari hii inaashiria kuanzishwa kwa njia ya kwanza ya moja kwa moja ya kusafirisha makontena kupitia baharini inayounganisha mji wa bandari wa kaskazini mashariki, Dalian na eneo hilo.

Njia hiyo mpya ya kusafirisha makontena iliyofunguliwa inajivunia kuwa na meli 11 kubwa zenye uwezo wa kubeba makontena 14,000 kila moja, zikiunganisha Mji wa Dalian na bandari kuu kadhaa za Ulaya, zikiwemo Gioia Tauro, La Spezia na Genoa nchini Italia, na Fos na Barcelona nchini Ufaransa na Uhispania, mtawalia.

Ikipita kwenye Njia ya Hariri ya Bahari ya Karne ya 21, njia hiyo ya meli pia inapitia nchi za Mashariki ya Kati kama vile Israel na Saudi Arabia.

Li Xiaoguang, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kituo cha Makontena cha Dalian, ambayo ni kampuni tanzu ya Kundi la Makampuni ya Bandari ya Liaoning amesema, kuanzishwa kwa njia hiyo kutanufaisha sana biashara kati ya eneo hilo na nchi za Ulaya. Hii itachochea ukuaji katika tasnia zao za ushindani, kama vile mashine na vifaa vya umeme, magari na vipuri vya magari, kemikali, madini, vyombo na mita, pamoja na nafaka na vyakula vilivyogandishwa kwa barafu.

"Hadi sasa, Bandari ya Dalian inaendesha njia 105 za usafirishaji wa makontena kwa njia ya bahari, zikiwemo njia 92 za biashara ya nje, ambazo zinajumuisha zaidi ya bandari 300 katika nchi na maeneo zaidi ya 160 duniani kote," Li ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha