Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang atoa wito kwa China na Ujerumani kupinga kwa pamoja "Vita Baridi Vipya"

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 10, 2023
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang atoa wito kwa China na Ujerumani kupinga kwa pamoja
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang (Kushoto) akipeana mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock wakati wa mkutano wao mjini Berlin, Ujerumani, Mei 9, 2023. (Xinhua/Ren Pengfei)

BERLIN - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang Jumanne alitoa wito kwa China na Ujerumani kushikilia kufuata njia sahihi, kupinga kwa pamoja "Vita Baridi vipya" na "kutenganisha uchumi wa nchi mbalimbali au kukata minyororo ya usambazaji bidhaa," na kuingiza imani na msukumo katika amani na ustawi wa Dunia.

Qin alisema hayo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock mjini Berlin.

China na Ujerumani zote ni miongoni mwa nchi kubwa zenye ushawishi wa kimataifa, Qin amesema, huku akibainisha kuwa nchi hizo mbili zinapaswa kuimarisha mazungumzo na ushirikiano chini ya hali ya sasa ya kimataifa inayoambatana na misukosuko.

"Pande hizi mbili zinapaswa kushirikiana kwa pamoja kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya duru ya saba ya mashauriano baina ya serikali ya China na Ujerumani, kukusanya mafanikio na kupanga mipango kabambe ya ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali siku zijazo," ameongeza Qin.

Amesema ili kukabiliana na masuala mbalimbali na changamoto mbalimbali katika dunia nzima, nchi zote zinapaswa kushirikiana badala ya kupambana, zinapaswa kuheshimiana badala ya kunyoosheana vidole.

Kwa upande wake Baerbock amesema Ujerumani inatilia maanani sana mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili pamoja na mabadilishano na ushirikiano katika sekta mbalimbali, na inatarajia kufanya duru ya saba ya mashauriano kati ya serikali za Ujerumani na China, ambayo yatakuwa mashauriano ya kwanza kufanyika nje ya mtandao baada ya janga la UVIKO-19 na ya kwanza kati ya serikali mpya za nchi hizo mbili.

Amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na China kwa ajili ya kupata matokeo yenye hamasa ya mashauriano hayo kuhusu kufanya juhudi za pamoja, uendelevu na hatua, hasa katika kuhimiza ushirikiano katika mabadiliko ya tabianchi, mageuzi ya nishati, viumbe anuai na mawasiliano kati ya vijana.

Pande hizo mbili pia zimebadilishana mawazo kuhusu suala la mgogoro wa Ukraine. Qin amefafanua msimamo wa China, akisisitiza kuwa msimamo thabiti wa China ni kuhimiza mazungumzo ya amani yafanyike, na kuhimiza jumuiya ya kimataifa kuunda msingi wa pamoja kwa ajili ya ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro huo. Amesema, nchi za Ulaya zilihimizwa kushughulikia dalili na sababu kuu za mgogoro huo, na kufanya juhudi za kurejesha amani na usalama.

Waziri Qin yuko ziarani nchini Ujerumani, Ufaransa na Norway kuanzia Mei 8 hadi 12 kwa mwaliko wa wenzake wa Ujerumani, Ufaransa na Norway.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha