Semina ya utangazaji wa Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji na Uuzaji Nje Bidhaa ya China (CIIE) yafanyika makao makuu ya AU

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 12, 2023

ADDIS ABABA - Semina ya utangazaji wa Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji na Uuzaji Nje Bidhaa ya China (CIIE), maonyesho ya biashara yanayofanyika kila mwaka huko Shanghai, China tangu Mwaka 2018, imefanyika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) siku ya Alhamisi.

Semina hiyo ya utangazaji, miongoni mwa mambo mengine, iliwakutanisha pamoja wawakilishi wa kamisheni ya AU, wanadiplomasia wa Afrika, kundi la wajumbe wa China, pamoja na wanadiplomasia kutoka Ujumbe wa China kwenye Umoja wa Afrika katika makao makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Wakati wa semina hiyo, wawakilishi kutoka ofisi ya maonyesho hayo waliujulisha upande wa Afrika kuhusu maelezo ya utangulizi kwa jumla kuhusu CIIE, maelezo ya utangulizi ya jumla ya maonyesho hayo kwa wahusika pamoja na uwezekano wa CIIE kuwezesha sekta binafsi na sekta ya umma ya Afrika kuingia katika soko pana la China.

Song Shangzhe, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Maonesho ya CIIE, alisema wakati wa semina hiyo kwamba kupitia CIIE, China kivitendo inachangia kuimarisha tena biashara ya kimataifa, ushirikiano wa kweli wa pande nyingi na uchumi wa dunia ulio wazi.

Kwa mujibu takwimu kutoka ofisi ya CIIE, nchi 31 za Afrika zilishiriki katika maonyesho ya tano ya CIIE, zikichukua eneo la maonyesho lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 2,000. Bidhaa za Afrika zimejitokeza katika CIIE, ambapo bidhaa kama vile kahawa, divai nyekundu, asali, pilipili hoho, na parachichi kutoka mataifa ya Afrika zimekuwa maarufu miongoni mwa watumiaji wa China.

Kwa upande wake Lin Zhiyong, Konsela wa ujumbe wa China katika Umoja wa Afrika, amesema ili kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Afrika, China imechukua hatua ya kupanua uagizaji wa bidhaa zisizo za rasilmali kutoka Afrika, kutoza ushuru sifuri wa forodha kwa asilimia 98 ya bidhaa kutoka nchi 33 za Afrika zenye maendeleo duni zinazouzwa China na kusaidia zaidi bidhaa za kilimo na viwanda za Afrika kuingia katika soko la China.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha