Mkuu wa UN wa masuala ya kibinadamu atoa wito wa kuongezwa muda wa mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 16, 2023
Mkuu wa UN wa masuala ya kibinadamu atoa wito wa kuongezwa muda wa mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths (kwenye skrini) akizungumza kwa njia ya video katika mkutano wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Mei 15, 2023. Griffiths Jumatatu ametoa wito wa kuongezwa muda wa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao unaruhusu Ukraine kuuza nafaka na bidhaa nyingine za kilimo nje ya nchi kutoka bandari za Bahari Nyeusi. (Eskinder Debebe/Picha ya UN/ Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA - Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths Jumatatu ametoa wito wa kuongezwa muda wa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao unaruhusu Ukraine kuuza nafaka na bidhaa nyingine za kilimo nje ya nchi kutoka bandari za Bahari Nyeusi.

“Chakula kinachouzwa nje chini ya mpango huo -- na mauzo ya chakula na mbolea kutoka Russia -- vinaendelea kutoa mchango muhimu kwa usalama wa chakula duniani kwani zaidi ya tani milioni 30 za mizigo zimesafirishwa kwa usalama kutoka Ukraine chini ya mpango huo,” Griffiths ameliambia Baraza la Usalama katika hotuba yake.

Amesema, mauzo hayo yanajumuisha takriban tani 600,000 za ngano zinazosafirishwa na Shirika la Mpango wa Chakula na Kilimo Duniani, katika kuunga mkono moja kwa moja shughuli za kibinadamu nchini Afghanistan, Ethiopia, Kenya, Somalia na Yemen.

Uchambuzi wa hivi punde wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)unaonyesha kuwa bei ya nafaka duniani imeshuka kwa karibu asilimia 20 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Mwezi uliopita, bei ya ngano katika soko la kimataifa ilifikia kiwango cha chini kabisa tangu Julai 2021, ikisukumwa kwa sehemu na kuendelea kusafirishwa kwa nafaka za Ukraine, na kupatikana kwa kiasi kikubwa kwa mauzo ya nje ya Russia na maeneo mengine, amesema Griffiths.

"Haya ni maendeleo yasiyopingika. Lakini bado kuna mengi zaidi ya kufanywa. Ugavi unaotabirika kwa ajili ya shughuli za chakula cha msaada wa kibinadamu unaendelea kuhitajika," amesema kupitia njia ya video kutoka Geneva.

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi ulitiwa saini katika maeneo tofauti na Russia na Ukraine huko Istanbul pamoja na Uturuki na Umoja wa Mataifa mnamo Julai 22, 2022. Mkataba huo, ambao ulianza kutumika kwa siku 120, uliongezwa muda wake katikati ya Novemba 2022 kwa siku 120 hadi Machi 18, 2023. Wakati huo, Russia ilikubali tu kuongeza mkataba huo kwa siku 60 zaidi, hadi Mei 18, 2023.

Griffiths amesema majadiliano ya ngazi ya juu bado yanaendelea kutafuta suluhu na namna ya kuongeza muda wake.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha