Waziri wa Mambo ya Nje wa China akutana na Naibu Waziri Mkuu wa DRC

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 23, 2023

https://english.news.cn/20230523/3bb768302b17461aa9503d5d20b22db8/5b64f66ce1014704bf29ee2687248e9e.jpg

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang akikutana na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Christophe Lutundula mjini Beijing, China, Mei 22, 2023. (Xinhua/Yan Yan)

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang Jumatatu alikutana na Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapa Beijing.

Akieleza kuwa China na DRC ni marafiki na ndugu wazuri wanaofurahia urafiki wa muda mrefu, Qin amesema China inakaribisha kwa furaha ziara iliyopangwa ya Rais Felix-Antoine Tshisekedi Tshilombo nchini China na anatarajia kwamba viongozi wakuu wa nchi hizo watafanya mipango ya hali ya juu na kubainisha mwelekeo wa kimkakati wa maendeleo ya uhusiano kati ya China na DRC katika hatua inayofuata.

Qin amesema kuwa China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara na chanzo cha uwekezaji kwa DRC kwa miaka mingi mfululizo. Amesema, China itaendelea kushirikiana na DRC ili kuendelea na ushirikiano wa hali ya juu katika ujenzi wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, kutekeleza makubaliano chini ya mfumokazi wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na kufikia ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.

“China iko tayari kuisaidia DRC kugeuza faida za rasilimali zake kuwa injini ya kuendesha maendeleo yake ya kiuchumi, na inatumai kuwa DRC inaweza kuweka mazingira mazuri ya biashara na kutoa dhamana ya usalama kwa wawekezaji wa China,” Qin amesema.

Amesema pande zote mbili zinapaswa kuimarisha mshikamano na uratibu katika masuala ya Umoja wa Mataifa na ya kimataifa, kulinda kwa uthabiti kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, na kwa pamoja kuendeleza utaratibu na usimamizi wa kimataifa wenye haki na usawa zaidi.

Kwa upande wake Lutundula ameishukuru China kwa msaada na uungaji wake mkono muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya DRC kwa miaka mingi, akisema kuwa DRC inashikilia kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja.

Amesema DRC itahimiza ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali na kuimarisha mawasiliano na uratibu na China ili kuleta manufaa zaidi kwa nchi hizo mbili na watu wao. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha