Waziri wa Mambo ya Nje wa China akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 24, 2023
Waziri wa Mambo ya Nje wa China akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA)
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang akikutana na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), mjini Beijing, China, Mei 23, 2023. (Xinhua/Ding Lin)

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang Jumanne alikutana na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), mjini Beijing.

Akisisitiza kuwa China inafuata kithabiti mkakati wa silaha za nyuklia wa kujilinda, Qin amesema kuwa China imejitolea kushikilia mfumo wa kimataifa wa kutoeneza silaha za nyuklia kwa kuzingatia Mkataba wa Kuzuia Kueneza Silaha za Nyuklia. Amesema China inaunga mkono kithabiti matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, inaimarisha kithabiti usalama wa nyuklia wa ndani na kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa kuhusu usalama wa nyuklia.

"China inatumai kuwa IAEA itafanya kazi zake kwa namna ya kufuata hali halisi, haki na kitaaluma, na kupinga kwa uthabiti mazoea ya nchi fulani kueneza dhana ya usalama wa nchi, na kuvuruga au kuathiri utaratibu wa kawaida wa ushirikiano wa kimataifa," Qin amesema.

Amesema, China pia inatumai kuwa IAEA itashughulikia ipasavyo suala la ushirikiano wa nyambizi za nyuklia kati ya Marekani, Uingereza na Australia, pamoja na Japan kutiririsha maji machafu ya nyuklia, na kulinda mamlaka na hadhi ya IAEA, mfumo wa kimataifa wa kuzuia kueneza nyuklia na usalama wa kimataifa.

Kwa upande wake Grossi amesema kuwa IAEA inatilia maanani sana ushirikiano na China, na inajitahidi kuzuia kueneza nyuklia. Grossi amesema IAEA itafanya mashauriano yanayofaa kuhusu ushirikiano wa nyambizi za nyuklia kati ya Marekani, Uingereza na Australia kwa njia ya uwazi, na haitaidhinisha utiririshaji wa maji machafu ya nyuklia kwenye bahari ya nchi yoyote.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha