Mtandao wa TikTok wafungua kesi mahakamani dhidi ya Jimbo la Montana la Marekani kupinga marufuku

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 24, 2023

https://english.news.cn/20230524/299a1015e3744ed7aeab8a9ea1b3d481/20230524299a1015e3744ed7aeab8a9ea1b3d481_3ecffeed-5f96-4ae7-9631-6422a2531572.jpg

Nembo ya Mtandao wa TikTok ikionekana kwenye skrini ya simu janja huko Arlington, Virginia, Marekani, Agosti 30, 2020. (Xinhua/Liu Jie)

LOS ANGELES - Mtandao wa kijamii wa TikTok umefungua kesi siku ya Jumatatu dhidi ya Jimbo la Montana la Marekani, ukitaka kubatilisha marufuku ya jimbo hilo dhidi ya programu hiyo ya kuchapisha video mtandaoni.

Hatua hiyo imekuja baada ya Gavana wa Montana Greg Gianforte kutia saini Mswada wa Seneti nambari 419 wiki iliyopita, na kuifanya Montana kuwa jimbo la kwanza la Marekani kupiga marufuku matumizi au ufikiaji wa mtandao huo wa kijamii.

"Tunapinga marufuku ya Montana isiyo ya kikatiba dhidi ya TikTok ili kulinda biashara yetu na mamia ya maelfu ya watumiaji wa TikTok huko Montana," imesema TikTok, yenye makao yake Los Angeles na inayojikita katika kuchapisha video fupi zilizotengenezwa na watumiaji, katika taarifa yake. "Tunaamini changamoto yetu ya kisheria itashinda kwa msingi wa kuwa na mifano na ukweli wenye ushawishi mkubwa."

Kesi hiyo ya TikTok, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani, inasema kwamba "kila mwezi, zaidi ya Wamarekani milioni 150 hutumia programu hiyo kujieleza na kuungana na wengine" na kwamba marufuku hiyo inakiuka Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani.

Kesi hiyo pia inasema kwamba Jimbo la Montana limepitisha baadhi ya "hatua za kushangaza na ambazo hazijawahi kuzingatiwa kwa msingi wowote zaidi ya uvumi usio na msingi."

"Ili kukomesha uamuzi huu usio halali, mlalamikaji anatafuta hukumu ya tamko na amri inayobatilisha na kumwagiza awali na kabisa Mshtakiwa kutotekeleza Marufuku dhidi ya TikTok," kampuni hiyo imesema katika malalamiko yake.

Kesi nyingine pia imefunguliwa dhidi ya Jimbo la Montana na watengeneza maudhui watano wa TikTok wiki iliyopita. Walalamikaji, ambao wana kazi mbalimbali, kama vile wanawake wa biashara, mfugaji, mwanafunzi na mkongwe, wote hutengeneza, huchapisha, hutazama, huwasiliana na kushiriki video za TikTok na "hadhira kubwa."

Wakati huo huo, Muungano wa Uhuru wa Kiraia wa Marekani ulituma ujumbe kwenye Mtandao wa Twitter wiki iliyopita kwamba "sheria hii inakanyaga haki zetu za uhuru wa kujieleza kwa kisingizio cha usalama wa taifa na kuweka msingi mkubwa wa udhibiti wa serikali kwenye Mtandao."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha