Waziri wa Mambo ya Nje wa China afanya mazungumzo na mwenzake wa Zimbabwe

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 30, 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang akifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Frederick Shava mjini Beijing, China, Mei 29, 2023. (Xinhua/Zhang Ling)

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang akifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Frederick Shava mjini Beijing, China, Mei 29, 2023. (Xinhua/Zhang Ling)

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Frederick Shava mjini Beijing siku ya Jumatatu, akitoa wito wa kuendeleza zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

Qin ameeleza kuwa China na Zimbabwe zimekuwa marafiki na washirika wazuri wanaoaminiana na kusaidiana tangu nchi hizo mbili zianzishe uhusiano wa kidiplomasia miaka zaidi ya 40 iliyopita. Amesema China iko tayari kushirikiana na Zimbabwe ili kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuunga mkono masuala yanayohusu maslahi ya msingi ya kila mmoja wao, na kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya China na Zimbabwe.

Amesema, kama ilivyofanya siku zote, China itaiunga mkono kwa dhati Zimbabwe katika kupinga uingiliaji kati na vikwazo kutoka nje, na kufuata njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi yake. Amesema, China itaongeza mabadilishano ya uzoefu na Zimbabwe katika utawala wa nchi.

“China itatumia fursa muhimu za ushirikiano na Zimbabwe katika nyanja kama vile uwekezaji, biashara, nishati na rasilimali za madini, nishati safi na maendeleo ya rasilimali watu, na itaendelea kuhimiza kampuni za China kuwekeza nchini Zimbabwe,” amesema Qin.

Kwa upande wake Waziri Shava akirejea kauli ya Qin, amesema uhusiano wa Zimbabwe na China umesimama kidete na kiwango cha ushirikiano wa kirafiki kimeboreshwa sana.

Amesema, Zimbabwe inashikilia kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na kuunga mkono kanuni ya "nchi moja, mifumo miwili", pamoja na Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia.

Amepongeza uungaji mkono mkubwa wa China kwa Zimbabwe katika kazi ya kupunguza umaskini na katika mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19. Ameeleza nia ya Zimbabwe ya kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana na China katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, na kuhimiza ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi hizo mbili kuendelezwa kwenye ngazi mpya. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha