Umoja wa Afrika wapitisha mpango elekezi wa kutatua mgogoro nchini Sudan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 30, 2023

Picha hii, iliyopigwa Aprili 15, 2023, ikionyesha moshi ukifuka Khartoum, mji mkuu wa Sudan. (Picha na Mohamed Khidir/Xinhua)

Picha hii, iliyopigwa Aprili 15, 2023, ikionyesha moshi ukifuka Khartoum, mji mkuu wa Sudan. (Picha na Mohamed Khidir/Xinhua)

ADDIS ABABA - Umoja wa Afrika (AU) umepitisha Mpango Elekezi wa Utatuzi wa Mgogoro nchini Sudan kuelekea kunyamazisha bunduki nchini Sudan.

AU imesema katika taarifa iliyotolewa Jumapili kuwa, mpango elekezi huo umepitishwa kwenye mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la AU ambao umehusisha viongozi wa ngazi ya wakuu wa nchi na serikali siku ya Jumamosi, ukiangazia hali ya Sudan.

Mpango elekezi huo unaainisha vipengele sita ambavyo ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa uratibu ili kuhakikisha juhudi zote za wahusika wa kikanda na kimataifa zinashabihiana na kuleta matokeo; kukomesha uhasama mara moja kwa kudumu, jumuishi na pande zote; na mwitikio mzuri wa hali ya kibinadamu.

Mkutano huo wa ngazi ya juu umesisitiza umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa mchakato mmoja wa amani, ambao ni jumuishi na shirikishi kwa Sudan, unaoratibiwa chini ya uratibu wa pamoja wa AU, Shirika la Maendeleo ya Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Mataifa na washirika wengine wenye nia moja.

"Baraza, kwa ufuatiliaji mkubwa wa karibu, linalaani vikali mgogoro usio na maana na usio na msingi unaoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF), ambao umesababisha hali mbaya ya kibinadamu isiyo na kifani, mauaji ya kiholela ya raia wasio na hatia," taarifa hiyo imesema.

Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali ya silaha kati ya SAF na wanamgambo wa RSF katika mji mkuu, Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15, huku pande hizo mbili zikilaumiana kwa kuanzisha mgogoro huo.

Kwa mujibu wa Muungano wa Madaktari wa Sudan, idadi ya raia waliofariki tangu kuanza kwa mapigano hayo imeongezeka hadi 863, huku kukiwa na majeruhi 3,531. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu hivi karibuni ilisema zaidi ya watu milioni 1 wameyakimbia makazi yao tangu mgogoro huo uanze.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha