Benki Mpya ya Maendeleo iliyoanzishwa na nchi za BRICS kuongeza ufikaji na ufadhili wa miradi kwa sarafu za nchi husika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 01, 2023

Picha iliyopigwa Juni 17, 2022 ikionyesha jengo la ofisi za makao makuu ya Benki Mpya ya Maendeleo (NDB) iliyoanzishwa na nchi za BRICS za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini katika Mji wa Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)

Picha iliyopigwa Juni 17, 2022 ikionyesha jengo la ofisi za makao makuu ya Benki Mpya ya Maendeleo (NDB) iliyoanzishwa na nchi za BRICS za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini katika Mji wa Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)

SHANGHAI - Benki Mpya ya Maendeleo (NDB) iliyoanzishwa na nchi za BRICS za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini itapanua ufikaji wake na kufadhili zaidi miradi yake kwa kutumia sarafu za nchi husika ili kusaidia maendeleo ya nchi zinazoibukia kiuchumi, Dilma Rousseff, mkuu wa benki hiyo, amesema Jumanne.

Rousseff ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa 8 wa mwaka wa NDB, ambapo ameorodhesha vipaumbele vya miaka michache ijayo, akisema kuwa benki hiyo inahitaji kupanua wigo wake, kuimarisha jukumu lake la kuwa jukwaa la ushirikiano.

“Benki hiyo itaongeza ushiriki wake katika shughuli za ufadhili wa pamoja na taasisi nyingine za kimataifa za kifedha, benki za maendeleo za kitaifa, na sekta ya kibinafsi,” Rousseff amesema.

Amesema NDB itakusanya fedha katika masoko mbalimbali ya dunia, na katika sarafu tofauti. "Wakati huo huo, tutatafuta kufadhili sehemu kubwa ya miradi yetu kwa sarafu za nchi husika, kwa malengo mawili ya kuimarisha masoko ya ndani ya nchi wanachama na kuwalinda wakopaji wetu dhidi ya hatari za ubadilishaji wa fedha."

Benki hiyo ina furaha kubwa kwa kuwa na wanachama wapya na kutakuwa na kasi ya upanuzi wa wanachama, Leslie Maasdorp, naibu mkuu na afisa mkuu wa fedha wa NDB, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano. "Kwa hivyo unaweza kutarajia kuona nchi nyingi zaidi zikijiunga kutoka maeneo mbalimbali duniani," amesema.

Mwaka 2021, NDB ilianzisha upanuzi, na kuzikubali Bangladesh, Misri, Falme za Kiarabu na Uruguay kuwa nchi wanachama wake wapya.

Ikiwa na makao yake makuu mjini Shanghai, NDB ilianzishwa na nchi za ushirikiano wa BRICS, ambazo ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Benki hiyo ilianza kufanya kazi rasmi Julai 2015.

Ikiwa ni sehemu ya kutoa huduma za uungaji mkono kwa taasisi zilizopo za kifedha za kimataifa na za kikanda, benki hiyo ilianzishwa ili kukusanya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu na miradi ya maendeleo endelevu katika nchi za BRICS, pamoja na nchi nyingine zinazoibukia na zinazoendelea, ili kuhimiza ukuaji wa uchumi na maendeleo duniani.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha