Sudan Kusini yasikitishwa na uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa vikwazo vya silaha dhidi yake

(CRI Online) Juni 01, 2023

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Bw. Deng Dau Deng, amesema nchi yake imesikitishwa na hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa vikwazo vya silaha dhidi yake na kuitaja hatua hiyo kuwa haina uhalali.

Bw. Deng amesema wanasikitishwa na kupinga hatua hiyo, ambayo wanaona imefanyika kwa nia mbaya, kwa kisingizio kuwa ni nchi yenye ukiukaji mwingi wa haki.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne lilipitisha azimio la kurefusha muda kwa mwaka mmoja hadi Mei 31, 2024, hatua za vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini, na vikwazo vilivyolengwa vya marufuku ya kusafiri na kuzuia mali za baadhi ya watu binafsi na mashirika.

Amesema vikwazo hivyo vinaathiri uchumi, biashara na usalama wa nchi. Na sasa bei za vitu zitapanda kwa sababu Sudan Kusini ni nchi isiyo na bandari na inategemea sana vitu vinavyoagizwa kutoka nchi jirani.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha