

Lugha Nyingine
Viongozi wa Afrika Mashariki wakiongezea muda kikosi cha kikanda huko mashariki mwa DRC
Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Jumatano mjini Bujumbura nchini Burundi, umeidhinisha kuongezewa muda wa miezi sita kuanzia Machi 8, 2023 hadi Septemba 8, 2023, kwa Kikosi cha Kikanda cha Afrika Mashariki ili kuimarisha mafanikio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Viongozi wa EAC waliidhinisha kwanza kutumwa kwa kikosi kipya cha kikanda Juni 20, 2022, lakini ni hadi ilipofika Novemba 2022 ndipo takriban wanajeshi 1,000 wa Kenya walitumwa kuwa kikosi cha kwanza cha wanajeshi kati ya vinne vilivyoahidiwa kufika Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki, wakuu wa nchi za EAC wamekipongeza kikosi hicho cha kikanda cha Afrika Mashariki kwa mafanikio yake katika kurejesha amani na usalama mashariki mwa DRC. Aidha wakuu wa nchi wamelaani vikali ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa DRC na kuagiza kikosi cha kikanda cha Afrika Mashariki kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo kujirudia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma