

Lugha Nyingine
Reli ya China-Laos yabeba bidhaa zinazovuka mpaka zenye uzito wa tani zaidi ya milioni 4
Makontena kwenye treni ya kwanza iliyobeba ndizi inayoelekea China kupitia Reli ya China-Laos yakionekana katika Stesheni ya Vientiane Kusini huko Vientiane, Laos, Desemba 6, 2022. (Picha na Kaikeo Saiyasane/Xinhua)
VIENTIANE - Shirika la Habari la Laos (KPL) limesema siku ya Alhamisi kuwa, reli ya China-Laos imesafirisha mizigo yenye uzito wa tani zaidi ya milioni 4 tangu ilipoanza kufanya kazi Mwaka 2021.
Shirika hilo limeripoti kwamba, tangu reli hiyo ilipozinduliwa Desemba 2021, treni za mizigo zilikuwa zimebeba bidhaa zilizoagizwa na kuuzwa nje ya nchi zenye uzito wa tani 4,097,300.
Kati ya kiasi hicho, takriban bidhaa zenye uzito wa tani 3,450,000 zilisafirishwa kutoka Laos hadi China na bidhaa zenye uzito wa tani 650,900 kutoka China hadi Laos.
Bidhaa zilizosafirishwa kutoka Laos hadi China zilijumuisha zaidi mpira, madini ya chuma, ore ya zinki, chokaa, matunda, unga wa viazi na shayiri. Wakati huo huo, bidhaa zilizosafirishwa kutoka China hadi Laos zilijumuisha vifaa vya umeme, vipuri na vifaa vya nyumbani.
Katika miezi mitano ya kwanza ya Mwaka 2023, mizigo yenye uzito wa tani 1,580,680 ilisafirishwa kutoka Laos hadi China, na bidhaa zenye uzito wa tani 160,910 zilisafirishwa kutoka China hadi Laos.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafanyabiashara nchini Laos, Thailand, Vietnam, Cambodia na Myanmar wanatumia Reli ya China-Laos kusafirisha bidhaa kutoka China na kwingineko.
Thailand inasafirisha mizigo inayoongezeka hadi China kwa njia ya reli, hasa mazao ya kilimo. Muda unaochukuliwa kusafirisha bidhaa kwa njia ya reli ni siku tatu, ikiwa ni kasi zaidi kuliko njia ya awali ya usafiri kwa barabara.
Reli ya China-Laos, ambayo ni mradi wa kihistoria unaoonyesha ushirikiano wa hali ya juu wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, ulianza kufanya kazi Desemba 2021. Reli hiyo ya kuvuka mpaka yenye urefu wa kilomita 1,035 inaunganisha Mji wa Kunming, Kusini Magharibi mwa China na mji mkuu wa Laos, Vientiane.
Picha hii iliyopigwa Januari 2, 2023 ikionyesha treni ya mwendokasi ya Lane Xang EMU ikiendeshwa kwenye sehemu ya Laos ya Reli ya China-Laos. (Picha na Yang Yongquan/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma