

Lugha Nyingine
Vikosi vya Idara ya Usalama na Usimamizi wa Sheria ya Uturuki vyakamata Biblia ya Kiebrania yenye umri wa miaka 1,100
Picha hii iliyopigwa Juni 12, 2023 ikionyesha nakala ya kale ya Biblia ya Kiebrania iliyokamatwa na Idara ya Usalama na Usimamizi wa Sheria ya Uturuki wakati wa operesheni huko Istanbul, Uturuki. (Picha na Omer Kuscu/Xinhua)
ISTANBUL - Vikosi vya Idara ya Usalama na Usimamizi wa Sheria ya Uturuki vimekamata nakala ya kale ya Biblia ya Kiebrania wakati wa operesheni ya kukomesha biashara haramu ya vitu vya kale vya kihistoria.
Nakala hiyo inaaminika kuwa yenye umri wa miaka 1,100, kwa mujibu wa taarifa ya Kamandi ya Vikosi vya Idara ya Usalama na Usimamizi wa Sheria ya Jimbo la Istanbul siku ya Jumatatu.
Vikosi hivyo vilifanya operesheni ya kusaka maeneo matatu baada ya kudokezwa kwamba washukiwa wanne walikuwa wakitafuta mnunuzi wa kitabu hicho kitakatifu chenye thamani ya dola 500,000 za Kimarekani.
Biblia hiyo ya Kiebrania iliwasilishwa kwa Taasisi ya Miswada ya Uturuki kwa uchunguzi zaidi, imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wakati wa operesheni hiyo, vikosi hivyo pia vilikamata sarafu 101 za zamani za enzi za Warumi na Byzantine, ambazo baadaye zilipelekwa Makumbusho ya Akiolojia ya Istanbul.
Washukiwa hao wanne walizuiliwa na kupelekwa katika mahakama moja iliyopo Istanbul.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma