

Lugha Nyingine
Reli ya China-Laos yarekodi safari 25,000 za abiria wanaovuka mpaka
![]() |
Treni ya abiria inayoelekea mji mkuu wa Laos, Vientiane ikiwa tayari kuondoka kutoka Stesheni ya Reli ya Kunming Kusini huko Kunming, Mkoa wa Yunnan, Kusini-Magharibi mwa China, Aprili 13, 2023. (Xinhua/Xing Guangli) |
KUNMING - Reli inayotoa huduma kati ya China na Laos imeshughulikia safari 25,000 za abiria za kuvuka mpaka tangu kuzinduliwa kwa huduma zake za abiria Aprili 13, kwa mujibu wa kituo cha ukaguzi wa mpakani cha Mohan.
Katika kipindi hicho, mji wa mpakani wa China wa Mohan katika Mkoa wa Yunnan, Kusini-Magharibi mwa nchi hiyo ulirekodi safari 14,156 za abiria wa ndani na safari za nje 11,752.
"Tunafurahi sana kusafiri kwa treni ya kimataifa ya abiria inayoendeshwa na Reli ya China-Laos, ambayo ni ya kustarehesha na rahisi," wamesema Michael na Alysha Dragoo, wanandoa kutoka Marekani. "Tunaweza kupanda treni hadi sehemu nyingi za Yunnan na Laos pia. Ni nzuri sana."
"Baada ya Reli ya China-Laos kuzindua huduma ya treni ya kimataifa ya abiria, kampuni nyingi za Laos zipo tayari kufanya biashara nchini China.
Mimi na rafiki zangu tunakwenda China wakati huu kuchunguza soko la longan," amesema Phoumy Sisaivong, mtalii kutoka Laos.
Reli ya China-Laos, ambayo ni mradi wa kihistoria wa ushirikiano wa hali ya juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, ilianza kufanya kazi Desemba 2021. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,035 inaunganisha Mji wa Kunming nchini China na Vientiane nchini Laos.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma