

Lugha Nyingine
Watu wote watano waliokuwemo kwenye chombo cha kuzamia majini cha Titan kutazama meli ya Titanic watangazwa kufariki
Picha ya kumbukumbu ya chombo cha kuzamia majini cha Titan. (Picha kwa hisani ya: OceanGate Expeditions)
OTTAWA - Walinzi wa Pwani wa Marekani wametangaza Alhamisi kwamba vifusi vilivyopatikana na watafutaji karibu na Meli ya Titanic mapema siku hiyo ni mabaki ya chombo cha kuzamia majini cha Titan ambacho kilikuwa kimebeba watu watano kwenda kutazama meli hiyo iliyozama ya Titanic.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari Alhamisi alasiri, Kamanda wa Walinzi wa Pwani ya Marekani John Mauger amesema chombo cha majini kinachoendeshwa kwa mbali (ROV) kiligundua mkia wa koni wa chombo hicho cha Titan karibu umbali wa nusu kilomita kutoka upinde wa Meli ya Titanic kwenye sakafu ya bahari.
"Baadaye ROV ilipata vifusi vya ziada. Kwa kushauriana na wataalamu kutoka ndani ya kamandi, vifusi hivyo vinaendana na upotevu mbaya wa chemba ya shinikizo," Mauger amesema.
"Natoa rambirambi zangu za dhati kwa familia," amesema.
Muda mfupi kabla ya tangazo hilo, OceanGate Expeditions, kampuni yenye makao yake makuu nchini Marekani ambayo inamiliki na kuendesha chombo hicho, ilisema katika taarifa yake kwamba inaamini kuwa abiria watano wa chombo hicho kilichokuwa kinakwenda chini ya maji kutazama Meli ya Titanic "kwa huzuni wamepotea."
Abiria hao watano ni pamoja na Hamish Harding, bilionea na msafiri wa safari za ugunduzi wa kijiografia; Paul-Henry Nargeolet, msafiri wa safari za ugunduzi wa kijiografia wa Ufaransa; Shahzada Dawood na mwanawe, Suleman Dawood, wanafamilia wa ukoo mashuhuri wa Pakistani; na Mkurugenzi Mtendaji wa OceanGate Expeditions na baharia wa Titan, Stockton Rush.
Chombo hicho cha kuzamia majini cha Titan kilipotea umbali wa zaidi ya kilomita 600 kutoka pwani ya Newfoundland mashariki mwa Canada mapema Jumapili asubuhi wakati kikizamia chini ya maji kuelekea kwenye eneo la ajali ya Meli ya Titanic kwenye Bahari ya Atlantiki Kaskazini.
Picha iliyotolewa Juni 21, 2023, ikionyesha Walinzi wa Pwani wa Marekani wakiendesha meli ya kutafuta chombo cha kuzamia majini cha Titan kilichotoweka karibu na eneo la ajali ya Meli ya Titanic. (Picha kwa hisani ya: Walinzi wa Pwani wa Marekani)
Juhudi za kimataifa za utafutaji zikiongozwa na Walinzi wa Pwani wa Marekani zilikuwa zikishindana na saa kutafuta chombo hicho ambacho kilikadiriwa kuwa na oksijeni yenye kuweza kutosha kwa saa 96 pekee ambayo ilitarajiwa kuisha Alhamisi asubuhi.
Kampuni ya OceanGate Expedition ilitumia chombo hicho cha watu watano kufikia eneo la ajali ya Meli ya Titanic umbali wa mita 3,800 chini ya uso wa bahari. Katika tovuti yake, kampuni hiyo inatangaza safari ya usiku saba kwenda kwenye eneo hilo kwa malipo ya dola za Kimarekani 250,000 kwa kila mtu na pesa zinazokusanywa kutoka kwa watalii hupelekwa kwenye utafiti wa Titanic.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma