Vyombo vya Habari vya Russia vyasema Makubaliano yamefikiwa kati ya Moscow na mkuu wa jeshi la Wagner

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 25, 2023

MOSCOW - Moscow na Yevgeny Prigozhin, mkuu wa kundi la kibinafsi la kijeshi la Wagner, wamefikia makubaliano kupitia upatanishi wa Rais wa Belarus Alexander Lukashenko jioni ya jana Jumamosi, kwa mujibu wa ripoti za shirika la habari la Russia, RIA Novosti.

Prigozhin amekubali pendekezo la Lukashenko la kusimamisha kusonga mbele kwa wanajeshi wa Wagner na kupunguza uchochezi wa hali, habari hiyo imesema.

Siku ya Jumamosi asubuhi, Rais Vladimir Putin wa Russia alimjulisha mwenzake wa Belarus juu ya hali ya nchini Russia kuhusu kundi la Wagner na wakuu hao wa nchi walikubaliana juu ya hatua za pamoja.

"Rais wa Belarus amefanya mazungumzo na Yevgeny Prigozhin.....Wamefikia makubaliano juu ya kutoruhusu kutokea kwa umwagaji damu wa watu wengi kwenye ardhi ya Russia," ofisi ya habari ya rais wa Belarus ilinukuliwa ikisema.

Kisha wapiganaji wa Wagner waliondoka eneo la Kusini mwa Russia la Rostov na kuelekea kwenye kambi zao, kwa mujibu wa shirika la habari la la Russia, TASS.

Kesi ya jinai dhidi ya Prigozhin itafutwa, na atakwenda Belarus, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari jioni Jumamosi, bila kutaja nini hasa Prigozhin atafanya katika nchi hiyo iliyokuwa sehemu ya nchi ya zamani ya Jamhuri ya Soviet Union.

Lukashenko amekuwa akifahamiana kibinafsi na Prigozhin kwa takriban miaka 20 na "hili lilikuwa pendekezo lake la kibinafsi lililokubaliwa na Putin," Peskov amesema.

"Kulikuwa na lengo la juu zaidi la kuepusha umwagaji damu, kuepusha mapambano ya ndani, kuepusha migogoro yenye matokeo yasiyotarajiwa. Imefanyika kwa ajili ya malengo haya kwamba juhudi za upatanishi za Lukashenko zilifanyika, na Rais Putin amefanya uamuzi ufaao," msemaji huyo amesema.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, hakikisho kwamba Prigozhin ataweza kuondoka kwenda Belarus limetolewa na rais wa Russia mwenyewe.

Ameongeza kuwa, tukio hilo na kundi la Wagner halitaathiri mchakato wa operesheni maalum ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine, ambayo itaendelea.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha