Mawimbi ya joto kali yaunguza maeneo ya Kaskazini mwa China huku tahadhari za halijoto kali zikitolewa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 26, 2023

Watalii wakijikinga na jua kali kwa miavuli kwenye Hekalu la Tambiko la Mbingu hapa Beijing, China, Juni 23, 2023.(Xinhua/Ju Huanzong)

Watalii wakijikinga na jua kali kwa miavuli kwenye Hekalu la Tambiko la Mbingu hapa Beijing, China, Juni 23, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)

BEIJING - Kuanzia Jumanne hadi Ijumaa, mawimbi ya joto kali yanatabiriwa kuunguza maeneo mbalimbali ya Kaskazini mwa China, maeneo kati ya Mto Manjano na Mto Huaihe, pamoja na Uwanda wa Fenhe-Weihe, kimesema Kituo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha China.

Maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Beijing-Tianjin-Hebei, Shandong, Henan, na Mongolia ya Ndani yatakuwa katika hatari ya kiwango cha kati cha madhara ya halijoto ya juu, kimesema kituo hicho.

Kituo hicho kimeshauri kuwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika maeneo yenye hali joto ya juu na watu wanaofanya shughuli za nje wachukue hatua muhimu za kujikinga, na kushauri idara husika kuhakikisha usambazaji wa maji na umeme.

Baadhi ya maeneo yaliyotajwa hapo juu yalipata halijoto ya juu kati ya Juni 21 na 24.

Halijoto katika kituo cha hali ya hewa kusini mwa Beijing ilipanda hadi nyuzi joto 41.1 saa 9:19 alasiri, Juni 22 – ikiwa ni kiwango cha pili cha juu zaidi cha joto kurekodiwa tangu rekodi za kuaminika kuanza kuchukuliwa, kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa ya Beijing.

Kituo cha uchunguzi wa hali ya hewa cha Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani wa China Jumamosi alasiri kilitoa tahadhari nyekundu, ambayo ni tahadhari kali zaidi kuhusu halijoto ya juu. Kiwango cha juu cha halijoto katika baadhi ya sehemu za mkoa huo kilipanda zaidi ya nyuzi 40 kati ya Ijumaa alasiri na Jumamosi alasiri.

Hali hiyo ya hewa ya joto inayoendelea, pamoja na ukosefu wa mvua wa kutosha, imeleta ukame mkali katika maeneo mengi ya mkoa huo.

Hadi kufikia Jumamosi, ukame umekumba eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 602,200, ikiwa ni asilimia 60.6 ya eneo lote la kilimo, misitu na ufugaji wa wanyama katika mkoa huo.

Mkoa wa Mongolia ya Ndani umetangaza hatua kadhaa za dharura za kukabiliana na ukame, kuimarisha ufuatiliaji wake wa ukame na kuchukua hatua kwa wakati kama vile shughuli za kurekebisha tabianchi.

"Tunapofanya kazi chini ya hali ya joto kali, lazima tuvae nguo za mikono mirefu, glavu na kofia ili kujikinga," amesema Pan Yulong mwenye umri wa miaka 29 anayefanya kazi katika Kundi la Kampuni la Shirika la Reli la China Tawi la Harbin.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha