Kenya na Iran zasaini mikataba 5 ili kukuza ushirikiano wa kivitendo katika sekta mbalimbali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 13, 2023
Kenya na Iran zasaini mikataba 5 ili kukuza ushirikiano wa kivitendo katika sekta mbalimbali
Rais wa Kenya William Ruto (Kulia) akipeana mkono na Rais wa Iran Ebrahim Raisi ambaye yuko ziarani barani Afrika wakati walipokutana jijini Nairobi, Kenya, Julai 12, 2023. Kenya na Iran zimetia saini nyaraka na makubaliano tano ya kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili siku ya Jumatano. (Picha na Fred Mutune/Xinhua)

NAIROBI - Kenya na Iran zimetia saini Nyaraka na makubaliano tano ya kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili siku ya Jumatano.

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini mbele ya Rais wa Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Kenya William Ruto mjini Nairobi, Kenya, yanahusiana na maeneo ya afya ya wanyama na uzalishaji wa mifugo, teknolojia ya habari na mawasiliano, uvuvi, utamaduni na urithi na kukuza uwekezaji.

"Makubaliano haya yataimarisha na kuongeza zaidi uhusiano wetu wa pande mbili kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu kati ya nchi zetu mbili," Rais Ruto amesema kwenye mkutano na wanahabari pamoja na Raisi baada ya kufanya mazungumzo.

Ruto amebainisha kuwa Kenya ilisafirisha chai yenye thamani ya dola milioni 28.31 kwenye soko la Iran katika robo ya kwanza ya Mwaka 2023, ambayo ni ongezeko la mara nane ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Rais huyo wa Kenya amedokeza kwamba kuanzishwa kwa Nyumba ya Ubunifu na Teknolojia ya Iran katika Mji wa Nairobi kutatoa jukwaa kwa biashara za Irani na Kenya.

Kwa upande wake Raisi amepongeza kujitolea kwa Kenya katika kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya biashara za kigeni, akibainisha kuwa nchi hizo mbili zina uwezo mkubwa wa kupanua ushirikiano wao wa pande mbili.

Amesema kampuni zaidi za Iran zitaanzisha shughuli zao nchini Kenya, zikifungua njia ya kufikia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, na masoko ndani ya mfumo wa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika.

"Uhusiano wa Kenya na Iran unaweza daima kuimarishwa kwa manufaa yetu," amesema Raisi ambaye amepanga kuzuru Uganda na Zimbabwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake barani Afrika, ambayo ni mara ya kwanza kwa Rais wa Iran katika kipindi cha miaka 11.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha