Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres asikitishwa na uamuzi wa Russia kukatisha makubaliano ya usafirishaji wa nafaka wa Bahari Nyeusi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 18, 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Julai 17, 2023. Guterres amesema Jumatatu amesikitishwa na uamuzi wa Russia kujiondoa kwenye  Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi. (Xinhua/Xie E)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Julai 17, 2023. Guterres amesema Jumatatu amesikitishwa na uamuzi wa Russia kujiondoa kwenye Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi. (Xinhua/Xie E)

UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Jumatatu kwamba amesikitishwa na uamuzi wa Russia kujiondoa kutoka kwenye Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

"Nasikitika sana uamuzi wa Shirikisho la Russia wa kusitisha utekelezaji wa Makubaliano ya usafirishaji wa nafaka wa Bahari Nyeusi, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa dhamana ya usalama ya Russia kwa usafiri kwenye bahari katika sehemu ya Kaskazini-Magharibi ya Bahari Nyeusi," Guterres amesema.

“Kwa uamuzi wa kusitisha utekelezaji wa Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, Russia pia imesitisha ahadi yake ya kuwezesha usafirishaji usiozuiliwa wa chakula, mafuta ya alizeti na mbolea kutoka bandari za Bahari Nyeusi zinazodhibitiwa na Ukraine, kama ilivyoonyeshwa katika makubaliano ya maelewano kati ya Russia na Umoja wa Mataifa,” ameuambia mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Guterre amesema makubaliano hayo yamehakikisha kupitishwa kwa usalama kwa zaidi ya tani milioni 32 za bidhaa za chakula kutoka bandari za Ukraine.

“Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limesafirisha zaidi ya tani 725,000 kusaidia shughuli za kibinadamu, kupunguza njaa katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi duniani, zikiwemo Afghanistan, Pembe ya Afrika na Yemen” amebainisha.

Ameongeza kuwa Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki - pamoja na makubaliano ya maelewano kati ya Russia na shirika hilo la dunia – yamekuwa tegemeo la usalama wa chakula duniani na mwanga wa matumaini katika Dunia yenye matatizo.

Mapema Jumatatu, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Moscow imeamua kusitisha ushiriki wake katika Makubaliano ya usafirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

"Kwa bahati mbaya, sehemu ya makubaliano haya ya Bahari Nyeusi ambayo inahusu Russia haijatekelezwa hadi sasa, kwa hiyo utekelezaji wake umesitishwa," vyombo vya habari vya Russia viliripoti, vikimkuu Peskov.

Makubaliano ya usaifirishaji wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambayo mwanzoni yalidumu kwa siku 120, yaliongezwa muda wake katikati ya Novemba 2022 kwa siku nyingine 120 hadi Machi 18, 2023. Kisha Russia ilikubali kuongeza muda kwa siku 60 pekee. Mei 17, Russia ilikubali kuongeza muda wa utekelezaji wa makubaliano hayo kwa siku nyingine 60.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha