Waziri Mkuu wa China Li Qiang akutana na John Kerry, mjumbe wa Marekani kuhusu suala la tabianchi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 19, 2023

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani kuhusu suala la Tabianchi John Kerry kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, China, Julai 18, 2023. (Xinhua/Ding Haitao)

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Marekani kuhusu suala la Tabianchi John Kerry kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, China, Julai 18, 2023. (Xinhua/Ding Haitao)

BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na John Kerry, mjumbe maalum wa Rais wa Marekani kuhusu suala la Tabianchi mjini Beijing siku ya Jumanne.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, Waziri Mkuu Li amesema China na Marekani zote ni nchi muhimu duniani, na kuimarishwa kwa ushirikiano kati yao kutanufaisha siyo tu nchi hizo bali pia Dunia nzima.

“Pande hizi mbili zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi hizi mbili kwenye mkutano wao uliofanyika Bali, Indonesia mwaka jana, ili kudhibiti ipasavyo tofauti na kuleta uhusiano wa China na Marekani kwenye njia thabiti na tulivu mapema iwezekanavyo” amesema.

Waziri Mkuu Li ameeleza kuwa mwitikio wa kimataifa kwa mabadiliko ya tabianchi ni kazi ngumu, ametoa wito wa kutekeleza ushirikiano wa pande nyingi na kushikilia malengo na kufuata kanuni zilizowekwa kwenye Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa na Makubaliano ya Paris. “Nchi zilizoendelea zinapaswa kuongoza katika kupunguza utoaji hewa chafu na kutimiza ahadi zao za kifedha haraka iwezekanavyo, na nchi zinazoendelea zinapaswa kutoa mchango kulingana na uwezo wao,” Waziri Mkuu Li amesema.

Pia ametoa wito wa kuchangia pamoja mafanikio ya kisayansi na kiteknolojia na kuhimiza mabadiliko ya kijani na utoaji kaboni chache, huku akizitaka nchi zilizoendelea kutoa usaidizi zaidi wa kiteknolojia kwa nchi zinazoendelea.

Kwa upande wake Kerry amesema Marekani inatumai uhusiano wa Marekani na China utaendelea kuwa tulivu. Na kwamba Marekani iko tayari kuimarisha ushirikiano na China ili kushughulikia kwa pamoja mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine kubwa za kimataifa na kuhimiza mafanikio ya Mkutano wa 28 wa pande zilizosaini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP 28).

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha