Wang Yi kuhudhuria mkutano wa BRICS na kutembelea nchi za Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uturuki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 20, 2023

BEIJING - Wang Yi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), atahudhuria Mkutano wa 13 wa Washauri wa Usalama wa Kitaifa na Wawakilishi Wakuu wa Usalama wa Kitaifa wa Ushirikiano wa Nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini (BRICS) huko Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia Julai 24 hadi 25, na kutembelea Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uturuki kabla na baada ya mkutano huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning ametoa taarifa hiyo Jumatano.

Taarifa hiyo imesema kuwa Wang, amealikwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Khumbudzo Ntshavheni wa Afrika Kusini na serikali za Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uturuki.

Akieleza kuwa mkutano wa washauri wa usalama wa taifa na wawakilishi wakuu wa masuala ya usalama wa taifa wa BRICS ni jukwaa muhimu kwa nchi za BRICS kufanya ushirikiano wa kisiasa na kiusalama, Msemaji Mao amesema China inatarajia kuwa na mazungumzo ya kina na washirika wa BRICS kuhusu hali ya sasa ya usalama wa kimataifa na masuala ya maslahi ya pande zote katika mkutano huo, kujenga maafikiano na kuimarisha ushirikiano, ili kuleta hamasa kwa Dunia inayokumbwa na misukosuko na mabadiliko, na kufanya maandalizi ya kisiasa kwa ajili ya Mkutano wa Viongozi wakuu wa BRICS utakaofanyika Agosti mwaka huu.

Katika wakati wa kuhudhuria mkutano wa BRICS, Wang atazuru Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uturuki katika safari hii.

“Ziara ya kutembelea nchi hizo inaonyesha ni kwa kiasi gani China inathamini uhusiano wake na nchi hizo,” Msemaji Mao amesema na kuongeza kuwa katika ziara hiyo, Wang atakuwa na mikutano na mazungumzo na viongozi wa nchi hizo nne na kubadilishana mawazo kwa mapana kuhusu uhusiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kimataifa na kikanda yenye maslahi kwa pande zote.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha