China iko tayari kuunganisha mkakati wa maendeleo na Brazil: Wang Yi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 25, 2023
China iko tayari kuunganisha mkakati wa maendeleo na Brazil: Wang Yi
Wang Yi (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akikutana na Celso Luiz Nunes Amorim (wa pili kushoto), mshauri mkuu wa Rais wa Brazil, mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Julai 24, 2023. (Xinhua/Zhang Yudong)

JOHANNESBURG - Wang Yi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amekutana na Celso Luiz Nunes Amorim, mshauri mkuu wa Rais wa Brazil, huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Kwenye mazungumzo kati yao yaliyofanyika siku ya Jumatatu, Wang amesema kuwa China na Brazil, nchi kubwa zaidi zinazoendelea katika nchi za Mashariki na Magharibi mwa Dunia, zina maslahi ya pamoja ya kimkakati.

Amesema China iko tayari kushirikiana na Brazil ili kuzidisha hali ya kuamiana kimkakati, kupanua ushirikiano wa kimkakati, na kuimarisha kuendana pamoja kati ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na mikakati ya maendeleo ya Brazil, kama vile kufufua viwanda na mpango wa kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.

"China pia iko tayari kushirikiana na Brazil kutafuta zaidi maslahi ya pamoja na kuanzisha vichocheo vya ukuaji wa uchumi, na kuufanya uhusiano kati yao kuwa kielelezo cha mshikamano na ushirikiano kati ya masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea, ili kuhimiza kwa pamoja maendeleo ya binadamu, na kujitahidi kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja," Wang amesema.

Amesema, mfumo wa ushirikiano wa BRICS umekuwa jukwaa wakilishi zaidi kwa ushirikiano wa Kusini na Kusini na unakabiliwa na fursa ya kihistoria ya maendeleo.

"China inapenda kuimarisha mawasiliano na uratibu na Brazil, kuhimiza kwa pamoja ushirikiano wa BRICS ili kuakisi ukweli mpya na kuitikia sauti za pande mbalimbali, kuendeleza kwa kuendana na wakati, kupata maendeleo mapya, kulinda vyema maslahi ya pamoja ya masoko yanayoibukia na nchi zinazoendelea, na kuhimiza dunia yenye ncha nyingi na demokrasia katika uhusiano wa kimataifa," amesema.

Kwa upande wake, Amorim amesema China ni mwenzi muhimu wa kimkakati wa Brazil, na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa na matokeo mazuri katika sekta mbalimbali.

Amesema, Brazil iko tayari kuimarisha ushirikiano na China katika mifumo kazi ya pande nyingi kama vile BRICS, kudumisha kwa pamoja ushirikiano wa pande nyingi na kulinda amani ya dunia.

Pande hizo mbili pia zimebadilishana mawazo kuhusu masuala ya kimataifa yanayofuatiliwa kwa pamoja.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha